Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), zimezindua Programu ya Utoaji Elimu kwa Umma kuhusu masuala ya fedha, inayolenga kuwajengea wanafunzi, wanufaika wa mikopo na jamii kwa ujumla uelewa na ujuzi wa kusimamia na kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
Uzinduzi wa programu hiyo umefanyika leo, Novemba 09, 2026, katika ofisi za Benki Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili iliyosainiwa mwezi Mei mwaka huu.
Awali, akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema dhamira ya Bodi haiishii katika kutoa mikopo na ufadhili kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na mahitaji, bali pia kuhakikisha wanufaika wanakuwa na uelewa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi, usimamizi na urejeshaji wa fedha za mikopo.
Dkt. Bill amesisitiza umuhimu wa wanafunzi wa elimu ya juu kuwa na ujuzi wa kusimamia fedha, ikiwemo kutimiza wajibu wa kurejesha mikopo kwa wakati ili kuhakikisha uendelevu wa mfuko na upatikanaji wa mikopo kwa vizazi vijavyo huku akiongeza kuwa HESLB itatumia mifumo mbalimbali kuwafikia walengwa.
Kwa upande wake Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Mhe. Emmanuel Tutuba, amesema uzinduzi wa programu hiyo ni sehemu ya juhudi za kuwajengea vijana uelewa wa masuala ya fedha ikiwa ni sehemu ya kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, katika kujenga uchumi imara na shindani kwa kuwapatia vijana na jamii ujuzi wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha.
Amesema kuwa kupitia ushirikiano huo, elimu ya usimamizi wa fedha itatolewa kwa wanafunzi kupitia akaunti zao za SIPA (Student’s Individual Permanent Account), huku maudhui yakiwa yameandaliwa ili kuwafikia wanafunzi kabla na baada ya kujiunga na vyuo.
Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, licha ya wanafunzi, elimu ya fedha itasaidia wazazi, walezi na wadau wengine wa elimu katika mafunzo yatakayohusisha upangaji wa bajeti, uwekaji akiba, upatikanaji wa kipato halali, matumizi yenye vipaumbele, uwekezaji na maandalizi ya kifedha baada ya kuhitimu.
Ameeleza kuwa maudhui yanapatikana kupitia tovuti za za BoT (www.bot.go.tz) na HESLB (www.heslb.go.tz ) ili kuwafikia pia wanafunzi ambao hawajapangiwa mikopo ya elimu ya juu, akisisitiza kuwa mafanikio ya programu yatapimwa kwa mabadiliko ya tabia za kifedha, hususan kujenga utamaduni wa kuweka akiba, kupanga bajeti na kutumia fedha kwa malengo yenye tija kwa maisha na maendeleo ya Taifa.
Gavana wa Benki Kuu amehitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa vijana kutumia fursa hiyo kujifunza na kujenga utamaduni wa kufanya maamuzi yenye tija kuhusu fedha wanazopata, huku akiwahimiza wadau wote kushiriki kusambaza elimu hiyo kwa jamii hususan wanahabari kutumia nafasi yao kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa elimu ya fedha.
Uzinduzi wa programu ya elimu ya fedha ulioandamana na uzinduzi wa video ya mafunzo na mwongozo wa utoaji elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na vya kati, ni hatua muhimu katika juhudi za BoT na HESLB kuimarisha uelewa wa masuala ya fedha nchini, hususan miongoni mwa vijana ili kuwajengea uwezo wa kutumia fursa za kifedha kwa tija, na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Taifa.