22
Nov 2026

SHIMMUTA 2026 YAFIKIA TAMATI, TAASISI 96 ZASHIRIKI

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Stephen Chaya, (Jumamosi, Novemba 21, 2026) amefunga rasmi Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Mashirika ya Umma, Taasisi na Makampuni Binafsi (SHIMMUTA 2026), katika Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro, yakishirikisha taasisi 96 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa taasisi zilizofanya vizuri ni Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ambayo imehitimisha ushiriki wake kwa mafanikio baada ya kutwaa nafasi ya pili katika mchezo wa mpira wa kikapu kwa wanawake, pamoja na kushinda nafasi ya tatu katika mchezo wa riadha wa kukimbia kwa magunia.

Mafanikio hayo kwa HESLB yanatokana na juhudi, nidhamu, mshikamano na ari ya ushindani iliyooneshwa na timu ya HESLB katika kipindi chote cha mashindano kwa kushiriki katika michezo mbalimbali.

Mashindano ya SHIMMUTA yaliyoanza Novemba 6, 2026, yameongozwa kwa kaulimbiu isemayo “SHIMMUTA 2026: MICHEZO ITUUNGANISHE KUELEKEA AFCON 2027”, ikiwa na lengo la kuimarisha mshikamano, umoja na ushirikiano miongoni mwa watumishi wa taasisi za umma na binafsi kupitia michezo, sambamba na kuhamasisha maandalizi ya Tanzania kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka ujao (AFCON 2027).

Akizungumza katika hafla ya kufunga mashindano hayo, Mhe. Dkt. Chaya, ambaye amemwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda, amesisitiza umuhimu wa mashindano ya AFCON 2027 kwa Tanzania, ikizingatiwa kuwa ni miongoni mwa nchi tatu waandaaji wa mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.

Dkt. Chaya ameeleza kuwa maandalizi ya AFCON 2027 yanahitaji ushiriki na mshikamano wa Watanzania wote, huku akihimiza michezo ya SHIMMUTA kuendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga umoja, kuimarisha afya na kukuza vipaji vya michezo miongoni mwa watumishi wa umma.

Hafla hiyo pia imepambwa na utoaji wa tuzo, medali na makombe kwa taasisi zilizofanya vizuri katika michezo mbalimbali iliyoshindaniwa ikilenga kutambua juhudi, uwezo na mafanikio ya washiriki.

Kwa ujumla, SHIMMUTA 2026 imekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano na ushirikiano baina ya taasisi za Serikali, kukuza vipaji vya michezo na kuhamasisha utamaduni wa mazoezi kwa lengo la kujenga afya bora na ustawi wa watumishi wa umma.

Kumalizika kwa mashindano ya SHIMMUTA 2026 mjini Morogoro, ni hatua muhimu katika kuendeleza mshikamano kupitia michezo na kutoa msukumo kwa Watanzania kuungana na kushiriki kikamilifu katika safari ya kuelekea AFCON 2027.

Published: November 22, 2026 at 12:14 PM