Higher Education Students' Loans Board
1. UTANGULIZI
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatangaza Programu ya Ufadhili iitwayo ‘SAMIA SCHOLARSHIP’ kwa masomo ya shahada ya awali kwa wanafunzi 1,000 waliopata ufaulu wa juu katika mitihani ya taifa ya kidato cha sita inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika tahasusi za sayansi (PCB, PCM, CBG, PGM, CBA, PMC na CBN).
Ufadhili wa ‘SAMIA SCHOLARSHIP’ utagharimia masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi hao ambao wameomba au kupata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba kwa kuzingatia ‘Mwongozo’ uliotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ambayo inasimamia utekelezaji wa ‘Scholarship’. Mwongozo huo unapatikana www.heslb.go.tz
2. SIFA ZA KUPATA UFADHILI
i. Awe Mtanzania,
ii. Awe na ufaulu wa juu (Daraja la kwanza, pointi 3 hadi 5) kwenye mitihani ya taifa ya kidato cha sita mwaka 2025 iliyoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) katika tahasusi za sayansi zilizotajwa. Aidha, kwa wale wenye mahitaji maalumu, wawe na ufaulu wa daraja la kwanza (pointi 3 hadi 9) katika tahasusi zilizotajwa,
iii. Awe amepata udahili katika Chuo cha Elimu ya Juu hapa nchini kinachotambuliwa na Serikali katika fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Sayansi za Tiba ambazo zimetajwa katika kundi la kwanza (Cluster 1) katika Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Shahada za Awali kwa mwaka wa masomo 2025/2026 unaopatikana www.heslb.go.tz,
iv. Awe ameomba ufadhili kwa usahihi kwa njia iliyoelekezwa,
v. Lazima awe miongoni mwa wanafunzi waliochaguliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa ajili ya kunufaika na ‘Scholarship’,
3. MAENEO YA UFADHILI
Ufadhili utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ya kugharimia maeneo yafuatayo:-
a. Ada ya Mafunzo
b. Posho ya Chakula na Malazi
c. Posho ya Vitabu na Viandikwa
d. Mahitaji Maalum ya Vitivo
e. Mafunzo kwa Vitendo
f. Utafiti
g. Vifaa Saidizi kwa Wanafunzi Wenye Mahitaji Maalum
h. Bima ya Afya
4. MUDA WA UFADHILI
Kwa wanafunzi waliopata ufadhili wa masomo kupitia ufadhili huu, ili kusoma shahada za awali watagharimiwa kwa muda wa kati ya miaka mitatu (03) hadi mitano (05) kulingana na programu husika walizodahiliwa.
5. UTARATIBU WA KUOMBA UFADHILI
Maombi ya ‘Samia Scholarship’ yatawasilishwa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao https://olas.heslb.go.tz kuanzia Julai 28 hadi Agosti 31, 2025. Wanafunzi watakaoruhusiwa kuomba ni wale ambao orodha yao imetangazwa kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz
Ili kuona majina ya wanafunzi waliopata ufadhili bofya hapa
6. WAJIBU/MASHARTI YA UFADHILI
Mwanafunzi atakayepata Ufadhili wa ‘SAMIA SCHOLARSHIP’ ana wajibu wa kuzingatia masharti yafuatayo:
a. Anapaswa kusoma, kuelewa na kusaini Mkataba wa Makubaliano ya Ufadhili kati yake na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
b. Anapaswa kuwa na akaunti ya Benki kwa ajili ya kupokelea fedha atakazolipwa moja kwa moja,
c. Mnufaika hataruhusiwa kubadilisha programu ya masomo aliyopatia ufadhili bila idhini ya maandishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,
d. Mwanafunzi mnufaika hataruhusiwa kuahirisha masomo, isipokuwa kwa sababu za kiafya, na kuthibitishwa kwa maandishi na chuo husika,
e. Ikiwa mnufaika ataghairi fursa ya ufadhili, atapaswa kuwasilisha taarifa ya maandishi kwenda kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu kupitia chuo alichodahiliwa na kusajiliwa,
f. Iwapo ufaulu wa mnufaika utashuka chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo, ufadhili wake utasitishwa.
7. MUHIMU KUZINGATIA
a. Ufadhili huu kikomo chake kitazingatia mwongozo wa ‘Samia Scholarship’ unaotolewa na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
b. Orodha ya majina ya wanafunzi husika inapatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz
c. Wanafunzi wote walioomba Samia Scholarship Extended (DS/AI+) wanaelekezwa kuomba pia Samia Scholarship kwa vyuo vya ndani ya nchi na waliomo katika orodha inayopatikana kupitia www.moe.go.tz na www.heslb.go.tz
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mtendaji
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
Julai 22, 2025
Taarifa hii pia inapatikana www.moe.go.tz na kurasa za mitandao ya kijamii za HESLB; Facebook, Instagram na X kwa jina la HESLB Tanzania