Higher Education Students' Loans Board
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, Mhe. Amir Mkalipa, leo ameongoza uzinduzi wa kitaifa wa zoezi la utoaji elimu kuhusu taratibu za uombaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2025/2026. Uzinduzi huo umefanyika katika ukumbi Rock City Mall jijini Mwanza na kushirikisha wadau mbalimbali wa elimu, wanafunzi, wazazi, watoa huduma za internet cafes na stationaries.
Akizungumza katika hafla hiyo ambayo wadau 1,012 wameshiriki, Mhe. Mkalipa ambaye amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda, ameelezea fahari kwa Mkoa wa Mwanza kuwa mwenyeji na kinara wa uzinduzi huo muhimu kitaifa na kuwa miongoni mwa mikoa 22 ambayo Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) itafanya zoezi hili la kutoa elimu kuanzia leo Julai 28 hadi Agosti 10, 2025.
“Hii ni heshima kubwa kwetu na inaonesha jinsi ambavyo Mkoa wa Mwanza unatambulika katika juhudi zake za kuhimiza elimu na maendeleo ya watu wake,” alisema Mhe. Mkalipa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Mhe. Mkalipa ameeleza kuwa uzinduzi huo sio tu ni ishara ya kujivunia, bali pia ni jukwaa muhimu la kutoa maarifa kwa wanafunzi na wazazi kuhusu namna ya kuomba mikopo kwa usahihi ili kuhakikisha waombaji wahitaji wanafikiwa na kuwawezesha, kwa kuwapangia mikopo ili kusoma vyuo vikuu. Hivyo amesisitiza wanafunzi, wazazi na walezi kujitokeza katika maeneo yote ambayo HESLB itapita, ili kupata elimu hiyo.
Aidha, katika hotuba hiyo, mgeni rasmi alieleza jinsi Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kuwekeza katika elimu ya juu. Alifafanua kuwa serikali imekuwa ikiiongezea bajeti kila mwaka ili kuwafikia watanzania wengi zaidi.
“Kwa mwaka wa masomo ulioisha wa 2024/2025, bajeti ya mikopo ya elimu ya juu ilikuwa TZS bilioni 787. Mwaka huu wa 2025/2026, bajeti hiyo imeongezeka na kufikia TZS bilioni 916. Hili ni ongezeko kubwa linalolenga kuhakikisha kuwa Watanzania wengi zaidi, hususan wale wa kipato cha chini, wanapata fursa ya kujiendeleza kielimu,” ameeleza Mhe. Mkalipa.
Mhe. Mkalipa pia amezungumzia jitihada nyingine za Serikali kama vile kuanzishwa kwa ‘Samia Scholarship’ tangu mwaka wa masomo 2022/2023, ambayo inalenga kuwahamasisha wanafunzi wanaosoma tahasusi za Sayansi kufanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA). Ameongeza kuwa tangu mwaka wa masomo 2023/2024, Serikali ilipanua wigo wa upatikanaji wa mikopo kwa kuanza kuwakopesha wanafunzi wa ngazi ya Stashahada (Diploma).
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia ameelezea umuhimu wa elimu hiyo kwa umma kuhusu taratibu za uombaji mkopo, kuwa huwasaidia wanafunzi na wazazi kuelewa vigezo, nyaraka muhimu na hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kukamilisha maombi kwa usahihi.
Dkt. Kiwia amewasihi wanafunzi, wazazi na walezi, pamoja na watoa huduma kama wa Internet Café na Stationeries, kushiriki kikamilifu kwenye zoezi hili la utoaji wa elimu, kwa kuuliza maswali, kuchukua taarifa muhimu na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma.
Mhe. Mkalipa amehitimisha hotuba yake kwa kuitaka HESLB pamoja na wadau wake ikiwemo Benki ya CRDB, kuhakikisha kuwa elimu ya uombaji mkopo wa elimu inakuwa endelevu na kuwafikia wananchi wengi zaidi katika mikoa yote nchini.
Uzinduzi huo, uliambatana na utoaji wa elimu na huduma kwa wananchi ambapo wataalamu kutoka HESLB waliwasaidia wananchi kujua hatua za uombaji mkopo, namna ya kupata namba ya kumbukumbu kutoka mfumo wa anwani za makazi (NaPA) na kujibu maswali ya moja kwa moja kutoka kwa wananchi.
Wanafunzi kutoka shule za sekondari Nsumba, Ngaza, Taqwa, Bwiru (Wavulana), Bwiru (Wasichana), Buswelu (Wasichana), Holy Family (Wasichana), Mwanza, Loreto (Wasichana), Messa, Lake, Rorya, na Pamba, walikuwa miongoni mwa washiriki.
Katika awamu hii elimu inatolewa katika mikoa ya Dodoma, Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Morogoro, mikoa mitatu ya Unguja, mikoa miwili ya Pemba, Mwanza, Kagera, Kigoma, Mbeya, Katavi, Njombe, Arusha, Tanga, Manyara, Mtwara, Ruvuma, na Lindi.