Higher Education Students' Loans Board
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Muhamed Mussa leo (Julai 17, 2025) amefungua rasmi Maonesho ya Sita ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi na kutembelea Banda la HESLB.
Mhe. Waziri Lela amepongeza kazi nzuri inayofanywa na HESLB kwenye utoaji wa elimu kuhusu utaratibu wa kuomba mikopo, taratibu za malipo vyuoni na urejeshaji wa mikopo.
Aidha, Mhe. Waziri amevutiwa na mpango wa ushirikiano baina ya HESLB na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma ya kufundishwa jinsi ya kupata namba za anwani za makazi (NaPA) inayotumika katika maombi ya mikopo yanayoendelea kwa mwaka 2025/2026.
“Hii ni njia sahihi ya kuwasaidia wadau na hasa wanafunzi hawa ambao wanaomba mikopo kipindi hikiwakijiandaa kujiunga na vyuo ”, amesema Waziri Lela.
HESLB inatoa huduma kwa wanafunzi wanaoomba mikopo, wazazi, walezi, wadau wa elimu na wananchi kwa ujumla wanaofika kwenye maonesho hayo yatakayofikia tamati tarehe 20, Julai, 2025.
HESLB imekuwa ikishiriki katika Maonesho ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar tangu yalipoanzishwa mwaka 2020 ili kutoa huduma za utoaji na urejeshaji mikopo ya wanafunzi.