Higher Education Students' Loans Board
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, leo Jumamosi, tarehe 19 Julai, 2025 ameshiriki kikamilifu kutoa huduma na elimu kwa wananchi kuhusu utoaji na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu katika Maonesho ya Sita ya Wiki ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika viwanja vya Mnazi Mmoja vilivyoko Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Pamoja na kutoa huduma katika banda la HESLB, Dkt. Kiwia amesisitiza umuhimu wa wanafunzi na wazazi kuelewa taratibu za kuomba mikopo, namna ya kufanya malipo vyuoni, na wajibu wa kurejesha mikopo kwa wakati.
Kupitia banda la HESLB, wananchi wamepata nafasi ya kuuliza maswali, kupata maelezo na ufafanuzi wa kina, na kujifunza kuhusu maboresho ya mfumo wa maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
Aidha, HESLB imeendeleza ushirikiano wa karibu na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutoa elimu juu ya matumizi ya Anwani ya Makazi (NaPA), ambayo ni kipengele muhimu katika mchakato wa maombi ya mikopo. Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa wanaoomba mikopo wanapata huduma kwa usawa na ufanisi.
Katika kuendeleza uhusiano na wadau wa elimu ya juu, Dkt. Kiwia alipata wasaa wa kutembelea mabanda mbalimbali, likiwemo la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB) ambapo alijadiliana na viongozi wa taasisi hiyo kuhusu masuala ya ushirikiano, kubadilishana uzoefu, na kuboresha mifumo ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa pande zote mbili za Muungano.
Ushiriki wa HESLB kwenye Maonesho ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar, ni sehemu ya juhudi za kuendeleza uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa mikopo, sambamba na kuhamasisha urejeshaji wa mikopo ili kuwezesha wanafunzi wengine wahitaji kupata fursa ya kugharimiwa masomo yao ya elimu ya juu.
Maonesho ya Sita ya Wiki ya Elimu ya Juu Zanzibar yaliyoanza tarehe 14 Julai, 2025 katika viwanja vya Mnazi Mmoja vilivyoko Mkoa wa Mjini Magharibi, yathitimishwa kesho Jumapili, tarehe 20 Julai 2025.
Hadi kufikia leo ikiwa ni siku ya sita ya maonesho hayo, takriban wageni 1,900 wamefika kutembelea na kupata huduma katika banda la HESLB.