Higher Education Students' Loans Board
Maonesho ya Kitaifa ya Kilimo (Nanenane) kwa mwaka 2025 yamezinduliwa rasmi leo Agosti 1, 2025 katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma, yakihudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ambaye amefungua rasmi maonesho hayo, ametoa wito kwa watanzania kutumia fursa ya maonesho kujifunza, kushirikiana na kuwekeza katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza uzalishaji na kukuza uchumi wa taifa.
Katika hotuba yake, Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa kuunganisha nguvu kati ya sekta ya elimu, tafiti na kilimo ili kuleta tija katika uzalishaji. Alieleza kuwa elimu na utafiti ni nguzo muhimu katika kuleta mapinduzi ya kilimo chenye tija na endelevu.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ni miongoni mwa taasisi zinazoshiriki kikamilifu katika maonesho haya kupitia banda la taasisi za kitaaluma na utafiti (Academic and Research Institutions).
HESLB inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali ikiwemo utoaji na urejeshaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, pamoja na elimu kuhusu usajili wa anuani za makazi (NaPA).
Wananchi wanaotembelea banda la HESLB wanapata fursa ya kuuliza maswali na kupata ufafanuzi wa kina kuhusu mchakato wa maombi ya mikopo, vigezo vya kupewa mkopo, namna ya kurejesha mikopo, na umuhimu wa kuwa na anuani sahihi za makazi kwa ufanisi wa utoaji wa huduma za kijamii.
Maonesho haya yataendelea hadi tarehe 8 Agosti 2025, na HESLB inawakaribisha wananchi wote kutembelea banda lao ili kupata elimu sahihi na huduma mbalimbali zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya elimu ya juu nchini.