Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo, Ijumaa Oktoba 03 2025, imehitimisha kikao kazi cha siku mbili kilichowakutanisha Menejimenti ya HESLB na Maafisa Mikopo kutoka vyuo vya elimu ya juu na vya kati nchini, kilichofanyika katika ukumbi wa Royal Tughimbe jijini Mbeya.
Akizungumza wakati wa kufunga kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwa Mikopo, CPA(T) George Mziray, alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza katika elimu ya juu kwa kutenga shilingi bilioni 916.5 kwa mwaka wa masomo 2025/2026, fedha zitakazonufaisha zaidi ya wanafunzi 252,000 nchini.
“Serikali imeweka kipaumbele katika elimu ya juu ili kuhakikisha kila kijana mwenye sifa na uhitaji anapata nafasi ya kusoma bila kikwazo cha fedha. Ni wajibu wetu kuhakikisha fedha hizi zinawafikia walengwa kwa wakati na kuwahudumia kwa uadilifu,” alisema Mziray.
Katika hatua nyingine, Bw. Mziray amewashukuru wadau mbalimbali wakiwemo Benki ya Azania, mdhamini mkuu wa kikao hicho pamoja na taasisi nyingine za kifedha kwa ushirikiano wao wa dhati katika kutoa huduma za kifedha kwa wanafunzi. Vilevile, aliwapongeza Maafisa Mikopo vyuoni kwa kazi kubwa wanayoifanya kama kiungo muhimu kati ya HESLB na wanafunzi waliopo vyuoni akisisitiza kuwa mashirikiano yaliyopo ndiyo msingi wa maboresho ya huduma bora.
Washiriki wa kikao hicho wameweka maazimio ya pamoja ikiwemo kuendelea kutumia mifumo ya TEHAMA ili kurahisisha huduma, kuongeza uwazi, na kupunguza malalamiko kutoka kwa wanafunzi.
Kikao hiki kimefungwa rasmi huku washiriki wakiahidi kutekeleza kwa vitendo maazimio yaliyofikiwa kwa manufaa ya wanafunzi na taifa kwa ujumla.