Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


8
December 2025

HESLB na ADAPT IT Zaingia Makubaliano Rasmi

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeingia katika hatua nyingine ya mageuzi ya kidijitali baada ya kuingia makubaliano rasmi na kampuni ya kimataifa ya TEHAMA, ADAPT IT ya Afrika Kusini, yenye uzoefu mpana katika kuendeleza mifumo ya elimu na fedha barani Afrika. Hafla fupi ya utiaji saini wa makubaliano hayo imefanyika leo, tarehe 8 Desemba, 2025 katika ofisi za HESLB kanda ya pwani, zilizopo jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na viongozi kutoka pande zote mbili.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mikopo ya elimu ya juu ili kuongeza ufanisi, uwazi na usalama wa taarifa. HESLB kwa miaka kadhaa imekuwa ikitekeleza mageuzi ya kidijitali ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi wanaoomba mikopo, mahitaji ya uwazi wa taarifa na kuimarisha mifumo ya urejeshwaji mikopo kwa wahitimu.

Kupitia ushirikiano huu, ADAPT IT itasaidia HESLB kuboresha mifumo ya kiteknolojia, kuboresha mifumo mipya inayowezesha urahisi wa kupata taarifa na kuboresha miundombinu ya usalama wa data. Hii ni hatua muhimu katika kulinda taarifa nyeti za wanafunzi na wahitimu, sambamba na kuboresha kasi ya utoaji huduma bora.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesisitiza kuwa uhusiano huo ni sehemu ya mkakati wa Bodi katika kuhakikisha huduma za mikopo zinatolewa kwa ufanisi zaidi, kwa kuzingatia kuwa ADAPT IT wana uzoefu mkubwa katika elimu ya juu wa kutoa huduma kwa nchi zaidi ya 41 duniani. “Tunaamini kwamba teknolojia ni msingi wa utoaji huduma bora… Ushirikiano huu na ADAPT IT utatuongezea uwezo wa kuhakikisha tunatoa huduma bora na kwa wakati, kupitia kufanya maboresho ya mifumo yetu kuwa ya kisasa zaidi, salama na rafiki kwa watumiaji”, amesema Dkt. Kiwia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji ADAPT IT Bw. Luxolo Rubushe, amesema kuwa wako tayari kutoa utaalamu, uzoefu na ubunifu utakaowezesha HESLB kupata mifumo yenye viwango vya kimataifa. “Tunashirikiana na vyuo mbalimbali katika nchi kama Kenya, Rwanda, Afrika Kusini, Namibia, Lesotho, Botswana, Ghana na nyingine nyingi ndani na nje ya bara la Afrika. Tupo tayari kushirikiana na HESLB kuleta mageuzi chanya kwa kutumia teknolojia. Ushirikiano wetu na HESLB ni fursa ya kushirikiana katika kuboresha huduma za mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na kusimamiwa nchini Tanzania,” amesema Bw. Rubushe.

Makubaliano hayo yanajikita katika maeneo muhimu yafuatayo:

     Kukuza ushirikiano kati ya HESLB na ADAPT IT kupitia majukwaa ya kidijitali kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa mikopo ya wanafunzi na uzingatiaji wa taratibu.

     Kutambua na kutekeleza shughuli za pamoja kama vile kampeni za uhamasishaji, suluhisho za kiteknolojia na kujenga uwezo kwa watumishi, na

     Kujifunza kuhusu fursa za ADAPT IT katika kupata suluhisho za teknolojia na kusaidia ajenda ya HESLB ya mageuzi ya kidijitali

Kupitia makubaliano haya, HESLB inatarajia kuongeza ufanisi wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, kuongeza kiwango cha makusanyo ya mikopo na kupunguza changamoto zinazotokana na ucheleweshaji wa taarifa au mifumo kukwama. Wanufaika wa mikopo, waajiri na wadau wengine pia watanufaika na mifumo iliyoboreshwa ambayo itawapa uwezo wa kufuatilia taarifa muhimu kwa urahisi.

Makubaliano kati ya HESLB na ADAPT IT ni hatua muhimu katika safari ya mageuzi ya kidijitali ndani ya sekta ya elimu ya juu nchini Tanzania. Ni hatua inayodhihirisha dhamira ya serikali katika kutumia teknolojia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuhakikisha rasilimali za umma zinasimamiwa kwa ufanisi.