Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


17
November 2025

Rais Samia afungua Bunge la 13 na kuahidi kuongeza mikopo ya wanafunzi

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amefungua Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma, (Ijumaa, Novemba 14, 2025) kwa hotuba iliyogusa maeneo mbalimbali likiwemo la mikopo ya elimu ya juu ili kukidhi ongezeko la wanafunzi wanaotarajiwa kudahiliwa katika vyuo na kampasi zilizopangwa kuwepo kila mkoa.

“Kama tulivyowaahidi wananchi, tutaongeza mikopo ya elimu ya juu, kwani kipindi hiki kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, tutakuwa na kampasi za vyuo vikuu kila mkoa”, amesema Rais Samia.

Awali katika hotuba yake, Mhe. Rais amesema, katika miaka mitano ijayo serikali itaanza utekelezaji kamili wa maboresho ya Sera ya Elimu inayosisitiza elimu ujuzi na kuweka mkazo zaidi kwenye masomo ya sayansi na hisabati (STEM) ili kuongeza wanasayansi wabobezi katika eneo la sayansi ya data, akili unde, sayansi ya kompyuta na teknolojia za viwanda.

Aidha Mhe. Rais Dkt. Samia amesema kuwa Serikali itatumia Mfuko wa ‘Samia Scholarship’ kusomesha wanasayansi ndani na nje ya nchi na kwamba hatua hiyo litakwenda sambamba na kukamilisha shule maalum za Sekondari za Wasichana za Sayansi na za vipaji za Wavulana katika kila mkoa.

“Tutatumia Mfuko wa Samia Scholarship kusomesha wanasayansi hawa ndani na nje ya nchi. Jambo hili litakwenda sambamba na kukamilisha shule maalum za Sekondari za Wasichana za Sayansi na zile za vipaji za Wavulana katika kila mkoa. Ili kuhakikisha mitaala na silabasi zetu zinatekelezwa kikamilifu, tutaunganisha kwa njia ya kidijiti shule za vijijini na mijini ili kubadilishana uzoefu na taarifa”, amebainisha Mhe. Rais Samia.

Mhe. Rais pia amegusia eneo la Ufundi stadi ambapo amesema Serikali itasimamia mpango wa kuhakikisha kila Wilaya ina chuo cha VETA chenye vifaa stahiki kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo.

Tangu alipoingia madarakani katika muhula uliopita mwezi Machi 2021, Rais Dkt. Samia ameidhinisha fedha kiasi cha TZS 3.67 Trilioni kilichotumika kusomesha wanafunzi zaidi ya laki tano. Katika kipindi hicho pia imeanzishwa fursa ya ‘Samia Scholarship’, mikopo ya wanafunzi wa ngazi ya Stashahada (Diploma) na kuongeza kiwango cha fedha za kujikimu kwa siku kutoka TZS 8,500/= hadi TZS 10,000/=.