Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) zimesaini makubaliano ya ushirikiano yatakayolenga kuelimisha na kuhamasisha wakazi wa eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kuhusu taratibu za maombi na urejeshaji wa mikopo ya elimu ya juu pamoja na manufaa yake kwa jamii.
Makubaliano hayo pia yanalenga kuwezesha ufadhili kwa wanafunzi wenye sifa wanaotoka katika jamii zilizo jirani na eneo la hifadhi na hivyo kuongeza upatikanaji wa fursa za elimu ya juu kwa vijana wa eneo hilo.
Akizungumza katika hafla fupi ya utiaji saini wa makubaliano hayo, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Abdul-Razaq Badru, amesema mpango huo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa ufadhili kwa wanafunzi wanaodahiliwa vyuoni kutoka katika jamii zinazozunguka Hifadhi ya Ngorongoro. “Tutaanza kwa kuwafadhili jumla ya wanafunzi 50 watakaodahiliwa kwenye fani za Sayansi ya Anga, Mali Kale na Akiolojia pamoja na Uhifadhi wa Wanyama Pori,” amesema Kamishna Badru.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amefafanua namna makubaliano hayo yatakavyotekelezwa, ikiwemo HESLB kupokea, kusimamia na kutumia fedha zitakazotolewa na NCAA kwa ajili ya kugharimia masomo ya wanafunzi husika. Aidha, utekelezaji wa jukumu hilo utafanyika kwa kuzingatia sera za HESLB, maelekezo ya NCAA na mwongozo wa pamoja ambao pande zote zimekubaliana. HESLB pia itabuni na kutekeleza kampeni maalum za uhamasishaji na elimu kwa jamii zinazozunguka eneo la hifadhi kwa kuzingatia lugha, tamaduni na mazingira ya kijiografia ya eneo hilo.
Mbali na hilo, Dkt. Kiwia amesema pia, HESLB itatoa nyenzo muhimu za taarifa ikiwemo vipeperushi, na miongozo vitakavyowawezesha waombaji kupata mwongozo unaoeleweka na wa moja kwa moja katika mchakato wao.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Jenerali (Mstaafu) Venance Mabeyo, amesema ongezeko la mapato kupitia sekta ya utalii limeiwezesha serikali kuona umuhimu wa kuanzisha mpango huo wa kuwasomesha wanafunzi wanaotoka jirani na eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa HESLB, Prof. Hamisi Dihenga, ameishukuru NCAA kwa hatua hiyo na kusisitiza kuwa mpango huo uwe mfano wa kuigwa na taasisi nyingine ili kuongeza vyanzo vya fedha za kugharamia elimu ya juu na kuwafikia Watanzania wengi zaidi wenye uhitaji.
Kupitia makubaliano haya, HESLB inakusudia kuhakikisha kuwa vijana wa eneo la Ngorongoro wanapata fursa sawa za elimu ya juu kama watanzania wengine, na hivyo kuchangia katika kujenga jamii yenye elimu, ustawi na maendeleo endelevu.