Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


2
October 2025

KIKAO KAZI CHA 14 CHA MAAFISA MIKOPO VYUONI CHAFANA MBEYA

Maafisa Mikopo takribani 200 kutoka vyuo mbalimbali nchini, leo wamekutana jijini Mbeya katika kikao kazi cha 14 kilichoandaliwa na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Kikao kazi hicho kilichofunguliwa rasmi na Dkt. Keneth Hosea, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kimefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Royal Tughimbe jijini Mbeya kikiwa na kauli mbiu: “Fedha Zaidi, Fursa Zaidi, Tuwahudumie Wanafunzi kwa Weledi.”

Akihutubia washiriki, Dkt. Hosea amewakumbusha maafisa mikopo kuhusu  dhamira ya serikali ya kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kusaidia wanafunzi wahitaji ili waweze kutimiza ndoto zao.

Aidha, Dkt. Hosea amewasisitiza viongozi wa wanafunzi katika taasisi za elimu ya juu na vyuo vya kati kushirikiana na ofisi za mikopo kubaini changamoto mapema na kuzitatua bila kusababisha taharuki.

“Nikiri wazi huduma mnazozitoa kwa wanafunzi si tu zinachangia ustawi wa elimu ya juu bali pia zinahakikisha utulivu na amani vyuoni ... ni wajibu wetu kuhakikisha kila mhitaji anapata msaada bila kuchelewa na kwa uwazi,” alisema Dkt. Hosea.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Bi. Devotha Chacha, ameeleza furaha yake kwa uamuzi wa HESLB kufanya kikao hicho mkoani Mbeya, akisisitiza kuwa ni fursa ya pekee kwa jiji hilo kuwa mwenyeji wa wadau muhimu wa elimu ya juu.

 “Tunatambua mchango mkubwa wa maafisa mikopo katika kuhakikisha fedha za umma zinasimamiwa kwa uadilifu na uwazi, nawaalika pia mtembelee vivutio vyetu vya utalii hapa Mbeya,” alisema Devotha ambaye pia ni Afisa Tawala wa Wilaya ya Mbeya.

Akitoa salamu kwa wadau wa elimu pamoja na tathmini ya namna Bodi inavyofanya kazi, Mwenyekiti wa Bodi ya HESLB, Prof. Hamisi Dihenga, alibainisha kuwa menejimenti imejipanga kuhakikisha mchakato wa upangaji mikopo kwa mwaka mpya wa masomo 2025/2026 utakuwa umekamilika wakati vyuo vitakapofunguliwa ifikapo mwezi Novemba, 2025.

“Tunataka fedha ziwafikie wanafunzi wote wenye sifa kwa wakati, ili wasikwame katika safari yao ya kitaaluma ... na katika hili sina mashaka kabisa na utendaji kazi wa HESLB,” amesema Prof. Dihenga.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alieleza kuwa kikao kazi hicho ambacho hufanyika kila mwaka, ni muhimu kwa lengo la kufanya tathmini ya utekelezaji wa mwaka wa masomo uliopita na kujiandaa kwa msimu mpya wa utoaji mikopo.

“Dhamira ya serikali ni kuwasaidia wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini. Ndiyo maana bajeti ya mikopo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 787 mwaka 2024/2025 hadi shilingi bilioni 916.5 kwa mwaka mpya wa masomo,” alisema Dkt. Kiwia.

Katika kikao kazi hicho cha 14 kati ya Menejimenti ya HESLB na maafisa mikopo wa vyuo, maafisa mikopo kutoka vyuo 25 wametambuliwa na kukabidhiwa ngao na vyeti kutambua utendaji kazi wao katika mwaka wa masomo 2024/2025. Baadhi ya vigezo vilivyozingatiwa ni pamoja na kuwasilisha kwa wakati taarifa muhimu za wanafunzi ikiwa ni pamoja na matokeo, maombi ya ada na kushughulikia maswali na malalamiko ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo na ‘Samia Scholaship’.