Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


19
June 2025

DKT. KIWIA: WAOMBAJI MIKOPO SOMENI NA KUZINGATIA MIONGOZO

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Dkt. Bill Kiwia amewasisitiza waombaji mikopo wote kwa mwaka wa masomo wa 2025/2026 kusoma na kuzingatia miongozo ya utoaji mikopo ili kuwasilisha maombi yao kwa usahihi.

Dkt. Kiwia ameyasema hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika leo (Alhamisi, Juni 19, 2025) katika ofisi za HESLB kanda ya mashariki zilizopo jijini Dar es salaam, ambapo ameweka wazi kuwa miongozo hiyo inapatikana kwenye tovuti ya HESLB (www.heslb.go.tz).

“Dirisha la maombi ya mikopo kwa mwaka wa masomo 2025/2026 lipo wazi toka Juni 15, 2025 hadi Agosti 31 mwaka huu. Uzoefu unaonesha kuwa waombaji mikopo wamekuwa hawazingatii taratibu wakati wa kufanya maombi yao…hivyo tunawasihi waombaji wote wasome miongozo iliyopo kwenye tovuti yetu kabla ya kuomba mkopo kwa kuwa ndiyo inaelezea sifa, vigezo na utaratibu wa kuomba mkopo kwa usahihi,” amesema Dkt. Kiwia.

Sambamba na hilo, Dkt. Kiwia ameelezea hatua pamoja na nyaraka muhimu za kuambatisha kwenye fomu ya maombi. “Nawasisitiza waombaji mikopo kutumia namba ileile ya kidato cha nne atakayotumia kuomba udahili wa chuo….kujisajili kwenye mfumo wa maombi ya mkopo na kuwasilisha nyaraka zote zilizoelekezwa kwenye miongozo ikiwemo namba ya uhakiki wa cheti cha kuzaliwa, akaunti ya benki yenye majina sawa na yale ya mwombaji yaliyopo kwenye vyeti vyake vya kitaaluma, kitambulisho cha mdhamini, pamoja na picha za mdhamini na mwombaji”. 

Katika mkutano huo pia, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala kutoka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Bw. Godwin Mkisi ameweka bayana kuhusu umuhimu wa mashirikiano yanayoendelea kati ya HESLB na TASAF katika kuwawezesha wanafunzi wanaotoka kwenye kaya maskini kuweza kupata mikopo ya elimu ya juu.

“Hadi sasa wanafunzi 11,524 wanaotoka kaya maskini wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu na kwa mwaka huu tunaamini idadi hii itaongezeka na hivyo kuziwezesha na kuzikomboa kaya kipato maskini kutoka kwenye hali duni ya maisha,” amesema Bw. Mkisi.

Kwa upande wake Bw. Kassim Ndumbo ambaye alimwakilisha Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) katika mkutano huo, ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kuongeza wigo na kutoa mikopo kwenye vyuo vya kati. “Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita kwa kuanza kutoa mikopo kwenye vyuo vya kati … NACTVET tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa HESLB ili kuhakikisha waombaji wote wa mikopo kutoka kwenye vyuo vya kati wenye sifa zinazoelekezwa kwenye miongozo wanakopeshwa na kuweza kutimiza malengo yao”, amesema Bw. Ndumbo.

Akizungumzia kuhusu jinsi HESLB ilivyojipanga kutoa huduma kwa waombaji mikopo, Dkt. Kiwia ameweka bayana namba ambazo zitatumiwa na kituo cha huduma kwa wateja cha HESLB ili kutoa msaada na maelekezo pale ambapo waombaji mikopo watakwama katika hatua za kujaza fomu zao za maombi ya mikopo.

“Pamoja na kuwa tuna ofisi za kanda ambazo wateja wetu wanaweza kufika na kupata huduma, kituo chetu cha huduma kwa wateja kitaendelea kuwasaidia waombaji mikopo wanaokwama kupitia kwenye namba ya 0736 66 55 33 na kupitia ujumbe wa WhatsApp tu kwa namba 0739 66 55 33 kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 10.00 jioni”, amesisitiza Dkt. Kiwia.

Katika hatua nyingine Dkt. Kiwia amezungumzia kuhusu ufadhili wa ‘Samia Scholarship’, kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya Sayansi kwenye mitihani ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ya kidato cha sita, ambapo Kwa mwaka huu 2025/2026, wanafunzi 700 watapatiwa ufadhili huo. Orodha ya wanufaika wa ‘Samia Scholarship’ itapatikana baada ya matokeo ya kidato cha sita kutangazwa ili wajaze fomu maalum kwa ajili ya kupata ufadhili huo.

Katika mwaka wa masomo 2025/2026, Serikali imetenga kiasi cha TZS 917 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya kati na vya elimu ya juu nchini, ambapo itawanufaisha wanafunzi 252,773, kati yao takribani wanafunzi 88,000 watakuwa  wa mwaka wa kwanza.