Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


1
July 2023

MAELEZO YA AWALI KWA WAOMBAJI MIKOPO KWA MWAKA 2023/2024

1.0    UTANGULIZI

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), itatangaza hivi karibuni ‘Mwongozo wa Utoaji Mkopo na Ruzuku kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa Mwaka wa Masomo 2023/2024’ utakaopatikana katika www.heslb.go.tz kuanzia Ijumaa, Julai 7, 2023.

Waombaji mkopo watarajiwa wanashauriwa kuusoma na kuuelewa mwongozo huo kabla ya kujaza fomu za maombi ya mikopo kupitia http://olas.heslb.go.tz ili kumwezesha mwombaji kujaza fomu kwa usahihi na ukamilifu.

2.0     MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KWA SASA

Wakati Mwongozo unakamilishwa, mwombaji mkopo aliyemaliza kidato cha sita (Form VI) au stashahada (diploma) anashauriwa kuzingatia mambo yafuatayo:

1. Kusoma kwa makini na kufuata taratibu za maombi zitakazoelezwa kwa kina katika Mwongozo utakaopatikana kuanzia Julai 7, 2023;

2. Kuhakikisha kuwa namba ya mtihani wa kidato cha nne atakayoitumia kuomba mkopo iwe sawa na anayotumia kuomba udahili wa chuo;

3. Waombaji ambao wamefanya mtihani wa kidato cha nne zaidi ya mara moja wahakikishe wanaorodhesha namba zote katika maombi yao kama itakavyoelekezwa na mfumo;

4. Kuhakikisha kwamba vyeti vya kuzaliwa/vifo vimethibitishwa na Wakala wa Usajili, Ufi­lisi na Udhamini (RITA) au wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA) kwa taratibu za taasisi hizi;

5. Kwa waombaji mkopo waliozaliwa nje ya nchi au waombaji ambao wazazi wao wamefariki dunia wakiwa nje ya nchi wanaambatanishe barua ya uthibitisho kutoka RITA;

6. Mwombaji ajaze fomu kwa ukamilifu na kuhakikisha maeneo yote yamesainiwa kabla ya kuziwasilisha HESLB kwa njia ya mtandao;

7. Kila mwombaji ahakikishe ana akaunti ya benki yenye majina yake yaliyotumika katika mtihani wa kidato cha nne. Akaunti hii ndiyo itakayotumika kumlipa mwanafunzi mkopo wake;

8. Mwombaji ahakikishe ana Namba ya Simu ya mkononi iliyosajiliwa na inayopatikana ambayo itatumika kumtaarifu hatua mbalimbali za maombi yake;

9. Waombaji wote wanashauriwa kutunza nakala ya fomu ya maombi ya mkopo waliyowasilisha HESLB kwa kumbukumbu na rejea pale itakapohitajika.

10. Dirisha la kuomba mkopo kwa njia ya mtandao litakuwa wazi kuanzia Julai 7 hadi Septemba 30, 2023.

3.0     SIFA ZA JUMLA

Kwa mwaka 2023/2024, sifa za jumla kwa waombaji mkopo ni zifuatazo:

1. Awe Mtanzania mwenye umri usiozidi miaka 35 wakati wa kuomba mkopo;

2. Awe amedahiliwa katika taasisi ya elimu ya juu yenye ithibati kikiwemo Chuo Kikuu Huria cha Tanzania;

3. Awe ameomba mkopo kupitia mfumo wa maombi ya mkopo (OLAMS);

4. Asiwe na chanzo kingine kinachogharimia masomo yake ya elimu ya juu;

5. Kwa mwombaji aliyewahi kunufaika na mkopo wa HESLB, awe amerejesha angalau asilimia 25 ya fedha ya mkopo aliokuwa amekopeshwa awali;

6. Awe amehitimu elimu ya kidato cha sita (ACSEE) au stashahada (diploma) ndani ya miaka mitano iliyopita, kati ya mwaka 2019 hadi 2023.

4.0     ANGALIZO

Taarifa hii inalenga kutoa maelezo ya jumla ya awali ili kuwawezesha waombaji mkopo kujiandaa. Hivyo, tunapenda kusisitiza waombaji mkopo kuusoma na kuuzingatia Mwongozo utakaotolewa Julai 7, 2023.

Imetolewa na:

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,

Jengo la PSSSF, Ghorofa ya Nne,

Barabara ya Makole,

S.L.P. 984,

DODOMA

Jumamosi, Julai 1, 2023