Higher Education Students' Loans Board
- Mikopo imeongezeka kwa 69.7%
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ( Ijumaa, Juni 27, 2025 ) amehitimisha Bunge la 12 katika hotuba yake iliyochukua takriban saa tatu na kubainisha mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya elimu hususan katika mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.
Katika sehemu ya hotuba yake kwa Bunge ikiwa ni utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano iliyopita, Rais Samia amesema kuwa katika kipindi hicho, mikopo ya wanafunzi imeongezeka sambamba na idadi ya wanafunzi na pia kuanzishwa kwa ‘Samia Scholarship’ na mikopo ya stashahada.
Chini ya uongozi wa Rais Samia, Serikali imeongeza bajeti ya mikopo kutoka TZS 464 bilioni mwaka 2020/2021 hadi TZS 787.4 bilioni mwaka 2024/2025 , likiwa ni ongezeko la aslimia 69% .
“…Serikali imeongeza mikopo ya elimu ya juu kutoka TZS 464 bilioni mwaka 2020/2021 hadi TZS 787.4 bilioni mwaka 2024/2025 … kutokana na hatua hii, idadi ya wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu imeongezeka kutoka wanafunzi 142,170 hadi wanafunzi 248,332 mwaka 2024/2025. Aidha, programu ya ufadhili inayojulikana kama ’Samia Scholarship’ imeanzishwa na hadi sasa imenufaisha wanafunzi 1,343 waliojikita katika masomo ya sayansi, Teknolojia, uhandisi, hesabu na afya”, amesema Mhe. Samia.
Rais Samia pia amezungumzia kuhusu mikopo ya stashahada iliyoanzishwa mwaka 2023/2024 na kusema kuwa, “… tumeanza kutoa mikopo katika ngazi ya stashahada kwa wanafunzi wanaosoma fani za kipaumbele zikiwemo afya, sayansi ya ufundi, ambapo TZS 19.95 bilioni zimetolewa kwa wanafunzi 7,534”, amebainisha Mhe. Rais Samia.
Kuhusu kuondoa tozo ya asilimia 6 ya kulinda thamani ya fedha ili kuwapa afueni walipaji, Rais amesema, “… Serikali imeondoa tozo za asilimia 6 kulinda thamani ya fedha ya mikopo ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu”.
Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amehitimisha hotuba yake kwa kutoa shukrani kwa wananchi na viongozi kwa ushauri na ushirikiano waliompatia ili kutekeleza majukumu yake katika kipindi chote tangu alipoingia madarakani miaka minne iliyopita. Kuhitimishwa kwa Bunge la 12 ni mwanzo wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza Rais Samia alihutubia Bunge Aprili 22, 2021 alipoingia madarakani baada ya kuapishwa Machi 19, 2021 kufuatia kifo cha mtangulizi wake Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021.