Wanafunzi 14 kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro wamenufaika na mfuko wa ufadhili wa masomo wa Ngorongoro Scholarship Fund katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Wanafunzi hao wametambulishwa katika hafla ya kukabidhiwa ufadhili na kupongezwa kwa kupata fursa hiyo katika hafla iliyofanyika leo, Novemba 07, 2026 katika ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), jijini Dar es Salaamna kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Baraza la Wafugaji Ngorongoro.
Tukio hilo ni kiashirio cha hatua muhimu ya Ushirikiano kati ya HESLB na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) katika ufadhili wa wanafunzi wanaotoka katika jamii zinazoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ambapo NCAA imeikabidhi HESLB mfano wa hundi yenye thamani ya TZS 100 milioni.
Akizungumza mbele ya washiriki wa hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, ameeleza dhamira ya HESLB ya kuimarisha ushirikiano na taasisi pamoja na wadau mbalimbali ili kuongeza fursa za elimu ya juu kwa Watanzania wengi zaidi kupitia mifuko ya ufadhili wa masomo.
Dkt. Kiwia amesema ushirikiano kati ya HESLB na NCAA ni mfano mzuri wa jinsi taasisi zinavyoweza kuunganisha nguvu na rasilimali katika kuhakikisha wanafunzi wenye sifa wanapata fursa ya elimu ya juu bila kuzuiwa na changamoto za kiuchumi.
Amesema HESLB imejipanga kuhakikisha fedha zilizotengwa na NCAA kwa ajili ya ufadhili wa wanafunzi hao 14 zinasimamiwa kwa kuzingatia taratibu, mifumo na miongozo iliyowekwa, ili ziwafikie walengwa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Aidha, amewahimiza wadau wengine, taasisi za umma na binafsi kujitokeza na kuiga mfano wa NCAA kwa kuanzisha ushirikiano na HESLB katika kufadhili elimu ya juu, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata fursa ya kujiendeleza kielimu.
Kwa upande wake, Kamishna wa NCAA, Dkt. Abdul-Razaq Badru, ameeleza kuwa ufadhili huo unalenga zaidi fani za uhifadhi wa wanyamapori na misitu, malikale na utalii, ambazo zinaendana na majukumu ya msingi ya taasisi hiyo ya uhifahi.
Amesisitiza kuwa mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu matatu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ambayo ni uhifadhi, utalii na maendeleo ya jamii, akibainisha kuwa elimu ni nyenzo muhimu ya kuwawezesha wananchi kupata njia mbadala za kiuchumi kupitia ajira na kujiajiri.
Akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan suala la ujumuishi, Dkt. Badru amesema NCAA inaendelea kutekeleza dhana hiyo kwa kuhakikisha jamii inayoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro inawezeshwa na kupata fursa mbalimbali za maendeleo, ikiwemo elimu ya juu. Akisisitiza kuwa ujumuishi ni muhimu katika kuhakikisha hakuna kundi la wananchi linaloachwa nyuma katika safari ya maendeleo ya taifa.
Dkt. Badru ameeleza kuwa anaamini wanufaika wa mfuko huo watakapohitimu masomo yao watapata fursa za ajira na kujiajiri, kuzalisha na kupata kipato kitakachowawezesha kuendesha maisha yao pamoja na kusaidia familia na jamii zao.
Awali, akielezea historia ya mfuko huo wa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Mratibu wa Miradi wa HESLB, Bi. Gertrude Alphonce amesema baada ya NCAA na HESLB kuingia katika ushirikiano wa kimkakati (Oktoba 2025), hatua mbalimbali zilifuatwa ili kuhakikisha mfuko huo unatekelezwa kwa ufanisi.
Amezitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kuandaa mwongozo wa utoaji wa ufadhili, kufanya zoezi la uhamasishaji na kutoa elimu kwa jamii kuhusu fursa hiyo, kufungua dirisha la maombi, kupokea maombi kutoka kwa waombaji na hatimaye kufanya mchakato wa kuwapata wanafunzi waliokidhi sifa za kunufaika na ufadhili huo.
Naye, Katibu wa Baraza la Wafugaji, Bw. James Moringe, amesema tangu mwaka 1994, NCAA imekuwa ikiwezesha jamii zinazoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kupitia mipango mbalimbali ya maendeleo.
Vilevile Moringe ameziomba HESLB na NCAA kuendelea kuimarisha ushirikiano wao ili kuwawezesha wanafunzi wengi zaidi hasa wa kike ili kupata fursa za elimu ya juu kupitia ufadhili wa masomo na mikopo ya elimu ya juu.
Dkt. Badru amehitimisha kwa kuwapongeza wanafunzi hao 14 waliofanikiwa kupata ufadhili na kuwataka kutumia vizuri fursa hiyo kwa kusoma kwa bidii ili waweze kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kuchangia maendeleo ya jamii yao na taifa kwa ujumla, akikazia kuwa NCAA itaendelea kujitahidi kuongeza fursa za ufadhili kupitia mfuko huo ili wanafunzi wengi zaidi kutoka ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro waweze kunufaika na kupata elimu ya juu katika fani mbalimbali.