21
Oct 2026

TAARIFA KWA UMMA

WANAFUNZI 90,235 WAPANGIWA MIKOPO NA RUZUKU YA TZS 284.73 BILIONI AWAMU YA PILI 2026/2027

Wamo wanufaika wa Ngorongoro Scholarship

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumatano Oktoba 21, 2026) imetangaza awamu ya pili ya orodha ya wanafunzi 90,235 wenye sifa ambao wamepangiwa mikopo na ruzuku yenye thamani ya TZS 284.73 bilioni kwa ajili ya mwaka wa masomo 2026/2027.

Orodha ya wanufaika iliyotangazwa leo inajumuisha wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na masomo waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu na vyuo vya kati.

Wanafunzi 25,630 wa Shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 82.31 bilioni, wanafunzi 3,445 wa Stashahada (Diploma) wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 9.25 bilioni, wanafunzi 417 wa Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 1.04 bilioni.

Aidha, wanafunzi 6,225 wanaoendelea na masomo wamepangiwa mikopo kwa mara ya kwanza yenye thamani ya TZS 20.38 bilioni na wanufaika wa Ngorongoro Scholarship wamepangiwa ruzuku yenye thamani ya TZS 66 milioni.

Orodha hiyo pia inajumuisha wanufaika wa mikopo wanaoendelea na masomo wakiwemo wanafunzi 47,670 wa shahada ya awali ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 153.16 bilioni na wanafunzi 6,834 wa stashahada ambao wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 18.50 bilioni.

Wanufaika waliopangiwa mikopo

Orodha ya awamu ya pili, inafanya idadi ya jumla ya wanafunzi 256,010 ambao wamepangiwa mikopo na ruzuku katika awamu ya kwanza na awamu ya pili yenye thamani ya TZS 820.4 bilioni.

Hatua zinazofuata

Bodi imekamilisha upangaji wa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza. Hata hivyo, wanafunzi ambao bado hawajapangiwa mikopo na wana taarifa za ziada kuwawezesha kukata rufaa, wanashauriwa kufanya hivyo kuanzia tarehe 25 Oktoba, 2026 dirisha la rufaa litakapofunguliwa.

Tunaendelea kupanga ruzuku kwa wanafunzi wapya wa Samia Scholarship; na wanafunzi wanaoendelea na masomo watapangiwa mikopo katika awamu zijazo kwa kadri tunavyopokea matokeo kutoka vyuoni.

Hitimisho

HESLB inawakumbusha waombaji wa mikopo na ruzuku wenye sifa kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ambao bado hawajapangiwa mikopo au ruzuku, kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia ‘SIPA’ wakati taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikopo na ruzuku zikiendelea.

Imetolewa na:

Mkurugenzi Mtendaji,

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,

Dar es salaam

Jumatano, Oktoba 21, 2026

Published: October 21, 2026 at 6:44 PM