Wadau wa mikopo ya elimu ya juu nchini, hususan wanufaika wa mikopo na ruzuku, wanatarajiwa kunufaika na huduma zenye ufanisi, ubora, uwazi na zinazotolewa kwa wakati kufuatia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kupokea rasmi cheti cha ithibati ya Mfumo wa Usimamizi wa Ubora wa Kimataifa wa ISO 9001:2015 kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi amekabidhi cheti cha ithibati ya kwa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia na kuhusisha ofisi nane (8) za HESLB ikiwemo Makao Makuu pamoja na ofisi za kanda.
Katika hotuba yake kabla ya makabidhiano, Dkt. Katunzi amesema ithibati ya kiwango cha ISO 9001:2015 ni msingi kuendelea kutoa huduma kwa viwango.
“Kuwa na cheti ni hatua moja na kukitunza ni hatua nyingine … hivyo endeleeni kuzingatia matakwa na kujiandaa na ithibati ya viwango vingine ikiwemo ya mifumo ya TEHAMA”, amesema Dkt. Katunzi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kukabidhiwa cheti, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB , Dkt. Bill Kiwia, amesema “ISO 9001:2015 ni kiwango cha kimataifa kitakachowezesha taasisi hiyo kutekeleza mifumo madhubuti ya usimamizi wa ubora, kuongeza ufanisi na kuimarisha uwajibikaji na kuahidi kusimamia utendaji wa kazi na utoaji wa huduma zinazokidhi viwango”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya HESLB Bw. Bahati Singa amesema kuingia katika kiwango cha ISO 9001:2015,na safari ya kufikia mafanikio hayo ilihusisha ukaguzi wa uthibitishaji uliofanywa ambapo HESLB Ilikidhi vigezo vya utoaji huduma bora, na kwamba kamati hiyo itaendelea kushirikiana na watumishi wote kusimamia utekelezaji wa mfumo huo na kudumisha utamaduni wa ubora ndani ya HESLB.
Hatua ya HESLB kuingia viwango vya kimataifa inalenga kuimarisha mifumo na taratibu za kazi ili kuboresha huduma za upokeaji na ushughulikiaji wa maombi ya mikopo, utoaji wa taarifa, na utatuzi wa changamoto zinazowakabili wanafunzi, wazazi na wadau wengine wa elimu nchini.