Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kushiriki kwenye ‘orientation’ katika baadhi ya vyuo vya elimu ya juu vilivyofunguliwa kwa mwaka wa masomo 2026/2027, kwa lengo la kutoa elimu kuhusu mikopo ya elimu ya juu na taratibu za kuzingatia katika kipindi chote cha masomo.
Zoezi hilo limeanza rasmi Jumatatu, tarehe 19 Oktoba 2026, ambapo hadi sasa HESLB imefikia wanafunzi 7,970 kwenye vyuo vitano, ambavyo ni Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT) kilichopo Mwanza, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kilichopo Morogoro, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kilichopo Zanzibar. Vingine ni Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTU) na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), vyote vipo Dar es Salaam.
Kupitia zoezi hilo, HESLB inatoa elimu kuhusu taratibu za mikopo, masharti na mambo muhimu ambayo wanafunzi wanapaswa kuzingatia ili kuendelea kunufaika na mikopo yao. Aidha, wanafunzi wanakumbushwa wajibu wao kama wanafunzi na wanufaika wa mikopo, ikiwemo kuzingatia taratibu zinazotolewa na HESLB na kutumia fedha za mikopo kwa malengo yaliyokusudiwa, hasa kugharamia mahitaji muhimu ya elimu na maisha yao ya chuoni.
Vilevile, zoezi hilo linatoa fursa kwa wanafunzi kuuliza maswali mbalimbali kuhusu mikopo yao, changamoto wanazoweza kukutana nazo na taratibu za rufaa na huduma nyingine zinazotolewa na HESLB. Maswali hayo yanajibiwa na kufafanuliwa ili kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu huduma za mikopo na kuwasaidia kuwa na elimu kuhusu matumizi na usimamizi wa fedha wanazopatiwa.
HESLB inasisitiza kuwa uelewa wa taratibu za mikopo au ruzuku na uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo ni muhimu katika kuhakikisha wanafunzi wananufaika ipasavyo ili kutimiza majukumu yao kama wanufaika.
HESLB inawasihi wanafunzi wote wanaonufaika na mikopo na ruzuku za elimu ya juu kuendelea kujitokeza na kushiriki kikamilifu kwenye vipindi vya ‘orientation’ vinavyoandaliwa na vyuo vyao ili kupata elimu sahihi kuhusu mikopo, wajibu wao na kuzingatia taratibu zinazotakiwa, ikiwemo matumizi sahihi ya fedha za mikopo.
Kupitia ushiriki wake katika programu hizi ambazo hufanyika kila mwaka wa masomo unapoanza, HESLB inaendelea kuimarisha utoaji wa elimu na mawasiliano kwa wanufaika wa mikopo kwa lengo la kuhakikisha wanapata uelewa kuwawezesha kutumia mikopo yao kwa ufanisi na kutimiza malengo yao ya kitaaluma.