- YATENGA TZS 1.06 TRILIONI KUFADHILI WANAFUNZI
Wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wamekutana na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kujadili mafanikio ya taasisi hiyo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita ikiwa ni pamoja na ongezeko la ufadhili kwa wanafunzi na mikakati ya kuhakikisha mfuko wa mikopo ya elimu ya juu unakuwa endelevu.
Mkutano huo umefanyika (Jumatatu, Oktoba 12, 2026), katika ukumbi wa hoteli ya King Jada, Dar es salaam ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amewaeleza wahariri kuhusu hatua zilizopigwa katika kupanua fursa za elimu ya juu, kuboresha huduma kwa wanafunzi na kuimarisha urejeshaji wa mikopo.
Dkt. Kiwia amesema Serikali imevunja rekodi kwa kutenga TZS 1.06 trilioni kwa mwaka wa masomo 2026/2027, fedha zinazotarajiwa kuwafadhili wanafunzi wasiopungua 300,000, ikilinganishwa na TZS 916.7 bilioni zilizotengwa mwaka 2025/2026 na kuwanufaisha wanafunzi 289,932.
Amesema awamu ya kwanza ya upangaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ina wanafunzi 165,775 ambao wamepangiwa ufadhili wenye thamani ya TZS 535.7 bilioni, wakiwemo wanafunzi 74,769 wa shahada ya awali waliopangiwa TZS 246.88 bilioni na wanafunzi 8,538 wa stashahada waliopangiwa TZS 22.9 bilioni.
Ameongeza kuwa upanuzi wa ufadhili kwa wanafunzi wa stashahada na programu maalumu kama Samia Scholarship ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata elimu na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira na maendeleo ya taifa.
Akizungumzia urejeshaji wa mikopo, Dkt. Kiwia amesema HESLB imekusanya TZS 235.5 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026, sawa na asilimia 107 ya lengo la kukusanya TZS 220 bilioni, kikiwa ni kiwango cha juu zaidi cha makusanyo tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB amesema bado kuna changamoto chache ikiwemo ya wanufaika ambao mikopo yao imeiva lakini hawajaanza kurejesha mikopo hiyo. Kiasi kinachodaiwa kutoka kwa kundi hilo kinakadiriwa kufikia TZS 800 bilioni.
Dkt. Kiwia ameongeza kuwa HESLB inaendelea kutumia kampeni za #Fichua na #KiduchuFreshTunasonga kuhamasisha urejeshaji, huku wanufaika wenye kipato kidogo wakipewa nafasi ya kuanza kulipa taratibu kulingana na uwezo wao.
“Pamoja na mafanikio niliyoyataja, ... bado kuna maeneo yanayohitaji kuboreshwa, yakiwemo mawasiliano na wanufaika, uwasilishaji wa taarifa sahihi kwa wakati na kuwafikia wadaiwa waliomaliza masomo, hususan wale wanaofanya kazi katika sekta isiyo rasmi”, amesema Dkt. Kiwia.
Katika kuboresha huduma, amebainisha kuwa HESLB kwa sasa inatumia mifumo ya kidijitali kwa asilimia 95 (95%); katika maombi, usimamizi na malipo ya mikopo, ikiwemo OLAMS, SIPA, HESLB App na DiDiS, pamoja na mifumo ya akili unde ya Bwanaboom na Bibiboom inayosaidia kujibu maswali ya wanafunzi na wananchi kwa haraka.
Ameviomba vyombo vya habari kuendelea kushirikiana na HESLB katika kuelimisha umma kuhusu fursa za ufadhili, taratibu za kuomba mikopo na wajibu wa wanufaika kurejesha fedha walizokopeshwa ili kuwawezesha wanafunzi wengine kupata nafasi ya kusoma.
Dkt. Kiwia amesema mafanikio ya HESLB katika miaka mitano iliyopita ni msingi wa hatua zinazofuata, akisisitiza kuwa uendelevu wa mfuko huo ni jukumu la pamoja la Serikali, taasisi za elimu, waajiri, wanufaika na wadau wengine.