WANAFUNZI 165,775 WAPANGIWA MIKOPO YA TZS 535.7 BILIONI
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), leo (Jumamosi, Oktoba 10, 2026) imetangaza Awamu ya Kwanza ya upangaji mikopo na ruzuku kwa jumla ya wanafunzi 165,775 yenye thamani ya TZS 535.7 bilioni.
Fedha hizo ni kwa ajili ya kugharimia wanafunzi wa stashahada, shahada ya awali, wanaoendelea na masomo, na wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship, waliodahiliwa katika vyuo mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Idadi ya wanufaika wa mwaka wa kwanza na kiasi cha fedha
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, imeeleza kuwa:
Wanafunzi 74,769 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS. 246.88 bilioni,
Wanafunzi 8,538 wa stashahada wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS. 22.9 bilioni, na
Wanafunzi 873 wa Samia Scholarship waliopangiwa ruzuku kiasi cha TZS. 4.5 bilioni.
Kwa wanufaika wanaoendelea na masomo; taarifa hiyo imeeleza kuwa:
Wanafunzi 79,115 wamepangiwa mkopo kiasi cha TZS. 252.4 bilioni,
Wanafunzi 1,554 wa stashahada wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS. 3.8 bilioni, na
Wanafunzi 926 wa Samia Scholarship waliopangiwa ruzuku kiasi cha TZS. 5.1 bilioni.
Aidha, Bodi ya Mikopo inawakumbusha waombaji wa mikopo na ruzuku ambao hawakupangiwa mikopo au ruzuku katika awamu ya kwanza, kuendelea kufuatilia taarifa za maombi yao kupitia 'SIPA' wakati taratibu za uchambuzi na upangaji wa mikopo na ruzuku kwa mwaka huu 2026/2027 zikiendelea.
Hivyo katika awamu hii ya kwanza HESLB imepanga jumla ya TZS 535.7 bilioni kwa wanafunzi 165,775 wakijumuisha wanafunzi wapya wa shahada ya kwanza, wanafunzi wa stashahada, wanufaika wa Samia Scholarship pamoja na wanafunzi wanaoendelea na masomo.
Kiasi cha Bajeti kwa mwaka 2026/2027
Itakumbukwa kuwa Serikali imetenga kiasi cha TZS 1.06 Trilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku ili kugharimia
Wanafunzi 292,463 wakiwemo wanafunzi 111,342 wa mwaka wa kwanza wa shahada ya awali.
Wanafunzi 24,978 wa Stashahada, wakiwemo wanafunzi 14,000 wa mwaka wa kwanza,
Wanafunzi 2,738 wa shahada ya awali wanaofadhiliwa kupitia Samia Scholarship, wakiwemo wanafunzi wapya 1,000, na
Wanafunzi 513 wa Stashahada ya Juu ya Sheria kwa Vitendo wakiwemo wapya 350.
Imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji,
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu,
Dar es salaam
Jumamosi, Oktoba 10, 2026