9
Oct 2026

Upangaji mikopo unategemea takwimu sahihi – Dkt. Kiwia

Wathibiti Ubora wa Shule nchini wametajwa kuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu inapangwa kwa ufanisi mkubwa ili kuwafikia wanafunzi wahitaji wenye sifa.

Akizungumza katika kikao kazi kati ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Wathibiti Ubora wa Shule kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema taarifa sahihi za wanafunzi zinahitajika ili kuwezesha kupanga vizuri rasilimali za serikali kwa Wanafunzi wenye sifa.

“Kwa HESLB, taarifa sahihi ni muhimu katika kuboresha uelewa wa mahitaji ya wanafunzi na kusaidia katika mchakato wa upangaji wa rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu … kwa kifupi, ubora wa taarifa una uhusiano wa moja kwa moja na ubora wa upangaji mikopo kwa usahihi”, amesema Dkt. Kiwia.

Aidha, Mkurugezi Mtendaji wa HESLB, amesema kuwa kutokana na umuhimu wa kada hiyo ya Wathibiti Ubora wa Shule; kuwe na kikao cha aina hiyo kila mwaka ili kuwezesha kupata fursa ya kufanya tathimini na kuboresha zaidi mbinu za upatikanaji wa takwimu za shule za sekondari.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa Shule kutoka WyEST, Dkt. Ephraim Simbeye, amesema kuwa Ushirikiano huo baina ya HESLB na Wathibiti Ubora wa Shule ni hatua sahihi kwa vile wote wako chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na hivyo takwimu zinazohitajika zinawezesha ufanisi wa hatua mbalimbali za elimu.

“Ushirikiano huu ni njia sahihi … hapa tumekaa kama akizungumza kutokana na kusimamia takwimu za shule za sekondari ambazo ni sehemu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia … sote tunafanya kazi moja kuhakikisha tunasonga mbele. Elimu bora inahitaji rasilimali na usimamizi ulio bora”, amesema Dkt. Simbeye.

Licha ya Wathibiti Ubora wa Shule, washiriki wengine kwenye kikao kazi hicho ambacho kimefanyika kwa mara ya kwanza, walikuwa Menejimenti na Watumishi wa WyEST na HESLB wakiwemo Maafisa TEHAMA na Maafisa Mikopo ambao wamewasilisha mahitaji na maeneo yanayohitaji kutumia takwimu za shule za sekondari ili kupanga mikopo.

Published: October 9, 2026 at 3:17 PM