Kikao kazi cha 15 kati ya Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Maafisa Mikopo zaidi ya 200 kutoka vyuo mbalimbali nchini, kimehitimishwa jana (Septemba 24, 2026), kwa msisitizo wa kuimarisha ushirikiano na matumizi ya mifumo ya kisasa katika utoaji wa huduma za mikopo.
Kikao kazi hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Gold Crest, jijini Mwanza, kiliwakutanisha wadau wa masuala ya mikopo ya elimu ya juu kutoka sekta mbalimbali, na kimekuwa jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto zinazowakabili Maafisa Mikopo pamoja na kuweka mikakati ya kuboresha huduma kwa wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao kazi hicho mgeni rasmi wa tukio hilo CPA(T)George Mziray, Mkurugenzi wa Urejeshaji na Urejeshwaji wa Mikopo HESLB, alisisitiza umuhimu wa kufungamanisha mifumo ya HESLB na vyuo, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kurahisisha upatikanaji na uhakiki wa taarifa pamoja na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Ufungamanishaji wa mifumo kati ya HESLB na vyuo ni muhimu katika kuhakikisha taarifa zinapatikana kwa wakati, kwa usahihi na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wanafunzi.” alisema Mziray.
Kufanyika kwa kikao hiki kila mwaka kunatoa nafasi kwa HESLB na vyuo kukutana, kubadilishana uzoefu, kutatua changamoto zinazojitokeza, kuhuisha uelewa wa taratibu za mikopo, na kujenga mfumo wa mawasiliano unaorahisisha huduma kwa wanafunzi.
Kikao kazi hicho cha 15 kilichokuwa na kauli mbiu isemayo, “Ushirikiano Imara, Huduma Bora: Tuwekeze kwa Wanafunzi”, kimehitimishwa kwa maafisa mikopo kupendekeza kuwa kikao kazi cha 16 kifanyike katika mkoa wa Dodoma.