23
Sep 2026

HESLB YAIMARISHA USHIRIKIANO NA MAAFISA MIKOPO

Maafisa Mikopo zaidi ya 200 kutoka taasisi za elimu ya juu na vyuo vya kati nchini wamekutana na Menejimenti ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Mwanza katika Kikao Kazi cha 15, kinacholenga kuimarisha ushirikiano na kuboresha utoaji wa huduma za mikopo kwa wanafunzi kuelekea kuanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027.

Imeelezwa kuwa Maafisa hao wana nafasi muhimu katika mchakato wa huduma za mikopo kwa kuwa ndio kiungo kati ya wanafunzi, taasisi za elimu ya juu na HESLB, hususan katika kuhakikisha taarifa za wanafunzi zinawasilishwa kwa usahihi na kwa wakati, pamoja na kusaidia kutatua changamoto zinazohusu mikopo katika ngazi ya vyuo.

Kikao hicho cha siku mbili kinafanyika tarehe 23 na 24 Septemba 2026, chenye kauli mbiu isemayo, “Ushirikiano Imara, Huduma Bora: Tuwekeze kwa Wanafunzi”, kina lengo la kujenga uelewa wa pamoja kuhusu taratibu na miongozo ya utoaji wa mikopo, matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA, uwasilishaji wa taarifa za wanufaika na namna bora ya kuwahudumia wanafunzi.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. CP Salum Hamduni, ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuongeza fedha zinazotengwa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

Amesema kwa mwaka wa masomo 2026/2027, Serikali imetenga TZS 1.06 trilioni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi, kutoka TZS 916.7 bilioni zilizotengwa mwaka wa masomo 2025/2026.

Kwa mujibu wa Mhe. Hamduni, ongezeko hilo linatarajiwa kuongeza idadi ya wanafunzi watakaonufaika na mikopo kutoka 252,773 mwaka wa masomo 2025/2026 hadi wanafunzi 292,463 mwaka 2026/2027, wakiwemo wanafunzi wapya zaidi ya 111,000.

“Serikali imetimiza wajibu wake, na ni jambo la kujivunia kwamba imekuwa ikifanya hivyo kila mwaka tangu Bodi ya Mikopo ilipoanzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita. Hivyo, wanafunzi mna wajibu wa kukumbushana juu ya kuhakikisha mnatumia fedha hizi kwa kusoma kwa bidii ili mpate elimu bora na kukamilisha malengo yaliyokusudiwa,” amesema Mhe. Hamduni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema Bodi imeendelea kuongeza wigo wa huduma za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, huku idadi ya wanufaika ikiendelea kuongezeka kila mwaka.

Amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita, HESLB imetoa jumla ya TZS 4.6 trilioni kwa wanafunzi, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 60 ya fedha zote zilizotolewa na Bodi tangu kuanzishwa kwake takriban miaka 22 iliyopita.

Dkt. Kiwia amewataka Maafisa Mikopo kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa HESLB zinakuwa sahihi na zinazingatia taratibu na miongozo iliyowekwa, ili kuhakikisha mwanafunzi anayestahili anapata huduma kwa haki na kwa wakati.

“Tunatambua kuwa bado kuna changamoto zinazohitaji ushirikiano wa pamoja kati ya HESLB na Vyuo. Baadhi ya maeneo tunayopaswa kuendelea kuyapa kipaumbele ni pamoja na uwasilishaji wa taarifa za wanufaika kwa wakati, matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA, mawasiliano kwa wanafunzi na utatuzi wa changamoto kwa wakati,” amesema Dkt. Kiwia.

Kikao Kazi hicho cha 15 kati ya HESLB na Maafisa Mikopo wa Vyuo ni sehemu ya jitihada za Bodi za kuimarisha ushirikiano na vyuo, kuboresha mifumo ya utoaji wa huduma na kuhakikisha wanufaika wa mikopo wanapata huduma kwa ufanisi, haki na kwa wakati.

Published: September 23, 2026 at 3:05 PM