7
Sep 2026

NAIBU KATIBU MKUU ELIMU AZINDUA BARAZA LA WAFANYAKAZI HESLB

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amezindua Baraza jipya la Wafanyakazi la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), akisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa watumishi katika kujadili masuala ya msingi yanayolenga kuboresha utendaji na ufanisi wa taasisi.

Uzinduzi huo umefanyika leo, tarehe 07 Septemba 2026, katika Hoteli ya Cate, Morogoro, ambapo pamoja na uzinduzi wa Baraza hilo, wajumbe wanashiriki mafunzo ya uelewa kuhusu majukumu na umuhimu wa Baraza la Wafanyakazi pamoja na kujadili hoja mbalimbali za wafanyakazi.

Akizungumza katika mkutano huo, Prof. Mushi amesema Baraza la Wafanyakazi ni jukwaa muhimu la ushirikishwaji linalowapa watumishi fursa ya kutoa maoni, kujadili changamoto na kupendekeza maboresho yanayoweza kuongeza uwajibikaji, nidhamu na tija katika taasisi.

“Baraza la Wafanyakazi ni sehemu kubwa sana ya ushirikishwaji wa wafanyakazi na kujenga umiliki wa pamoja wa shughuli za taasisi. Ni jukwaa la kutoa maoni na kuboresha utendaji ili kuongeza uwajibikaji, nidhamu na tija ya pamoja, amesema Prof. Mushi.

Amesema pia, Baraza hilo lina nafasi muhimu katika kuhakikisha kuwa maslahi ya mwajiri na wafanyakazi yanalindwa kwa pamoja, pamoja na kusaidia katika usuluhishi wa masuala yanayoweza kujitokeza baina ya pande hizo mbili.

“Baraza ni jukwaa muhimu la kuhakikisha maslahi ya mwajiri yanalindwa, lakini wakati huo huo maslahi ya wafanyakazi nayo yanalindwa. Ni sehemu ya kuhakikisha usuluhishi unafanyika na maslahi ya pande zote mbili yanazingatiwa, amesema Prof. Mushi.

Prof. Mushi amesisitiza kuwa watumishi ndio rasilimali muhimu zaidi katika taasisi, na ametoa rai kwa Menejimenti ya HESLB kuendelea kuweka mkazo katika ustawi wao kwa kuwaendeleza kitaaluma, kuboresha maslahi yao na kuhakikisha masuala yanayowaathiri yanashughulikiwa kwa wakati ili kuongeza ari na tija kazini na amewataka wajumbe kujenga hoja, kusikilizana na kushirikiana ili kufikia malengo ya HESLB na kutoa huduma bora kwa Watanzania.

Aidha, ameitaka HESLB kuendeleza utendaji wake mzuri kwa kuzingatia uwajibikaji na uadilifu, akieleza kuwa Wizara ina jukumu la kutunga sera, wakati taasisi zilizo chini yake zina wajibu wa kutekeleza sera hizo kwa ufanisi kwa manufaa ya wananchi.

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amebainisha kuwa Baraza la Wafanyakazi lina umuhimu mkubwa katika kujenga mazingira bora ya kazi na kuwezesha watumishi kushiriki katika mijadala inayohusu ustawi wao na maendeleo ya taasisi.

Dkt. Kiwia amesema miongoni mwa mambo muhimu yatakayofanyika katika kikao hicho ni mafunzo ya uelewa kuhusu Baraza la Wafanyakazi, pamoja na kujadili hoja mbalimbali za wafanyakazi, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ufanisi na katika mazingira mazuri.

Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuongeza bajeti inayowezesha Watanzania kupata fursa ya elimu ya juu na elimu ya kati kupitia mikopo na ufadhili.

Prof. Mushi pia ameiagiza HESLB kufikiria njia bunifu na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu namna bora ya kuongeza upatikanaji wa fedha zaidi za kuwezesha wanafunzi wengi kupata mikopo, sambamba na kuendelea kutumia mifumo ya teknolojia kurahisisha utoaji wa huduma na kuhakikisha mikopo inatolewa kwa usahihi.

Amesema matumizi ya teknolojia yanapaswa kuendelea kupewa kipaumbele ili kuongeza ufanisi, kupunguza changamoto katika utoaji wa huduma na kuhakikisha wanafunzi wanapata huduma kwa wakati.

Baraza hilo la Wafanyakazi la HESLB linalojumuisha Menejimenti na wawakilishi wa wafanyakazi, linalenga kuimarisha ushirikiano kati ya Menejimenti na wafanyakazi, kuboresha mazingira ya kazi na kushughulikia hoja za watumishi kwa pamoja.

Published: September 7, 2026 at 11:25 AM