24
Aug 2026

HAFLA YA KILELE CHA WIKI YA KITAIFA YA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU 2026 YAFANA

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba leo (Agosti 24, 2026) amehitimisha Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, huku akisisitiza umuhimu wa elimu, ujuzi na ubunifu katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Maadhimisho hayo yalianza Agosti 15, 2026, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo: “Elimu, Ujuzi na Ubunifu ni Njia ya Kufika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Awali, akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamewashirikisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya elimu, ujuzi na ubunifu, ambapo zaidi ya taasisi 90 zimeshiriki kikamilifu.

Miongoni mwa taasisi hizo ni Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), ambayo imeshiriki kwa kutoa elimu kwa wananchi na wadau 1,869 kuhusu utaratibu sahihi wa kuomba mikopo ya elimu ya juu pamoja na namna ya kurejesha mikopo iliyoiva, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wanafunzi, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla wanafahamu taratibu na wajibu wao katika mikopo ya elimu ya juu.

Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 imekuwa pia fursa kwa taasisi mbalimbali kuonesha shughuli, huduma, bunifu na mafanikio yao, pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu mchango wa elimu, ujuzi na ubunifu kwa maendeleo ya Taifa.

Published: August 24, 2026 at 5:53 PM