Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imepata tuzo ya mshindi wa kwanza wa Banda Bora la Sekta ya Elimu katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es salaam (DITF) maarufu Sabasaba.
Tuzo hiyo imekabidhiwa leo (Julai 13, 2026) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Mhe. Shariff Ali Shariff, aliyekaimu nafasi ya Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda (SMZ); na kupokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia.
Utoaji wa Tuzo ulikuwa sehemu ya hafla ya ufungaji wa Maonesho ya 50 ya DITF ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE), inayosimamia Maonesho hayo, ambayo pia yametumika kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 ya DITF, Dkt. Latifa Mohamed Khamis amesema yalikuwa na mafanikio makubwa kwa ubunifu, biashara na huduma zilizotolewa kuanzia Juni 28, 2026.