Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeshiriki katika Imbeju Smart Elite Career Day iliyofanyika tarehe 27 Julai 2026 katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano kati ya HESLB, CRDB Bank Foundation na kampuni ya Basil Link.
Tukio hilo liliwakutanisha zaidi ya wanafunzi 400, wakiwemo wanaotarajia kujiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati katika mwaka wa masomo 2026/2027. Lengo kuu lilikuwa kuwajengea uwezo wa kupanga mustakabali wao wa kitaaluma kwa kuwawezesha kuelewa masuala muhimu yanayohusu; uchaguzi sahihi wa kozi za masomo, taratibu za uombaji wa mikopo ya elimu ya juu, vigezo na sifa za kupata mkopo, mchakato wa utoaji wa mikopo na wajibu wa urejeshaji wa mikopo baada ya kuhitimu masomo.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Meneja wa Utoaji Mikopo HESLB, Bw. Godfrey Chawe alisisitiza kuwa maombi ya mikopo hufanyika kupitia mfumo wa mtandao, hivyo waombaji wanapaswa kujaza na kufuatilia maombi yao kwa umakini badala ya kuyaachia watu wengine katika vituo vya huduma wanavyotumia kujaza fomu za maombi ya mkopo.
Aidha, alieleza kuwa HESLB inashirikiana na Shirika la Posta Tanzania kuwasaidia waombaji wa mikopo, sambamba na kuwepo ofisi saba za kanda za HESLB na Kituo cha Huduma kwa Wateja (Call Centre), ambao wanatoa msaada kwa waombaji wanaokumbana na changamoto wakati wa mchakato wa maombi.
Katika tukio hilo, HESLB pia iliweka dawati la huduma kwa wateja lililotoa elimu, ushauri na msaada kwa washiriki kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Bodi.
HESLB inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanafunzi wanapata taarifa sahihi kuhusu mikopo ya elimu ya juu na kuwezeshwa kupanga vyema mustakabali wao wa kitaaluma.