Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imeandaa mafunzo ya uombaji wa mikopo kwa usahihi kwa waliohitimu kidato cha sita, kidato cha nne au shashahada yatakayofanyika maeneo mbalimbali ya nchi kuanzia tarehe 20 hadi 29 Mei, 2026.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kutoa elimu ya kina kwa wanafunzi, wazazi na walezi kuhusu taratibu za kujaza fomu za maombi ya mkopo na kufafanua kuhusu nyaraka muhimu zinazohitajika ili kukamilisha maombi ya mkopo kwa usahihi.
Wadau wengine wa kimkakati watakaoshiriki katika utoaji huo wa elimu ni pamoja na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Usajili Ufilishi na Udhamini (RITA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), Shirika la Posta na Kampuni ya Simu Yas Tanzania.
Katika utoaji wa elimu, miongoni mwa huduma zitakazotolewa papo hapo ni pamoja cheti cha kuzaliwa, Namba ya Utambulisho wa Taifa, Elimu ya Mlipa Kodi na TIN namba, anwani ya makazi, huduma za kibenki na huduma ya Internet.
Wanafunzi, wazazi na walezi wanaolengwa wanahimizwa kushiriki katika maeneo yaliyotajwa kwenye matangazo kuhusu uombaji wa mikopo kwa mwaka 2026/2027. Awamu ya kwanza inaanza tarehe 20 hadi 30 Mei, 2026 na awamu ya pili itakayoendelea tarehe 25 hadi 29 Mei, 2026.