Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ipo katika Maonesho ya Elimu ya Juu yanayoendelea katika Uwanja wa Gombani, Pemba ikitoa elimu na huduma kuhusu utoaji na urejeshaji wa mikopo.
Katika Maonesho hayo yanayovutia mamia ya wananchi, HESLB inashirikiana na maafisa kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kitengo cha Anwani za Makazi (NaPA) na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Miongoni mwa wageni ni viongozi na wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu ambao wanaendelea kumiminika kwenye banda la HESLB na wadau wake kupata elimu ya jinsi ya kuomba mkopo kwa usahihi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Mhe. Khadija Salum Ali, Julai 24, 2026 alitembelea banda la HESLB na kupata maelezo ya utoaji wa elimu ya mikopo ya wanafunzi na huduma shirikishi hususan za kuwawezesha waombajj mikopo kwa mwaka 2026/2027 kuelewa sifa, vigezo na taratibu za kuomba mkopo kwa usahihi.
Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Chakechake Mhe. Zuhura Mgeni Othman alitembelea banda la HESLB (Julai 23, 2026) na kuipongeza kwa kuhakikisha changamoto nyingi za uombaji mikopo zinatatuliwa ndani ya banda moja baada ya kuona maafisa wa NIDA na NaPA wakiendelea kutoa huduma ndani ya banda la HESLB.
Maonesho hayo ya siku 5 yenye kauli mbiu “Ubunifu na Taaluma ni Msingi wa Maendeleo”, yalianza Julai 23 na yatahitimishwa Julai 27, 2026 katika Uwanja wa Gombani, Pemba.