14
Mar 2026

HESLB Yaandaa Futari na Wadau, Yasisitiza Kuchangia Elimu ya Juu

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Jumamosi ya Machi 14, 2026, iliandaa futari maalum iliyowakutanisha wadau mbalimbali katika Hoteli yaa Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, ambapo Mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Lazaro Londo.

Katika hotuba yake kwenye hafla ya Futari hiyo, Mhe. Londo alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ina dhamira thabiti ya kuendelea kuimarisha sekta ya elimu, hususan elimu ya juu, ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa. Alibainisha kuwa katika kutekeleza azma hiyo, Serikali imeendelea kuongeza bajeti kwa ajili ya kusomesha wanafunzi wa elimu ya juu kupitia mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo.

Aidha, alitoa wito kwa wanufaika wa mikopo wenye kipato kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa uaminifu ili kuwapa nafasi wanafunzi wengine kunufaika pia. “Wanufaika wa mikopo wanawajibika kuwa waaminifu kwa kurejesha mikopo pindi wanapopata kipato ili kuwawezesha na wengine,” alisema Mhe. Londo na kusisitiza kuhusu umuhimu wa taasisi mbalimbali kushirikiana katika kusaidia juhudi za kugharimia elimu ya juu nchini, “Ni muhimu taasisi za umma na binafsi kushirikiana maana tunaposhirikiana tunaweza kufanya mambo mengi mazuri na yatakayodumu kwa muda mrefu,”.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia wakati akitoa utambulisho na kuwashukuru kwa dhati waalikwa wote waliohudhuria, alisisitiza kuhusu umuhimu wa mashirikiano na wadau kutoka taasisi za serikali na binafsi katika utekelezaji wa majukumu ya HESLB. Amebainisha kuwa, mchango na ushirikiano wa wadau hao una nafasi kubwa katika kuimarisha juhudi za serikali za kugharimia elimu ya juu na kuwajengea vijana uwezo wa kitaaluma.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB, Prof. Hamisi Dihenga, akiongea kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, alitumia jukwaa hilo kuwasihi wadau mbalimbali kujitokeza kushirikiana na HESLB katika kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu, ikiwemo kupitia utoaji wa ufadhili wa masomo (Scholarships).

Prof. Dihenga alieleza kuwa tayari kuna taasisi ambazo zimeanza kuonesha nia ya kushirikiana na HESLB katika kusaidia wanafunzi na akatoa mfano wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ambayo imekubali kuanza kufadhili wanafunzi 50 wa vyuo vikuu.

“Nia yetu ni kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais katika juhudi za kuimarisha elimu ya juu nchini. Tupo tayari kushirikiana na wadau wengine kama ambavyo tumeshakubaliana na NCAA ambao wao watafadhili wanafunzi 50 wa vyuo vikuu, tunaomba wadau wengine pia wajitokeze tuwasaidie vijana wetu,” alisisitiza Prof. Dihenga.

HESLB imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa kimkakati kwa lengo la kuboresha utendaji wake pamoja na kufanikisha utoaji na urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu, hatua inayochangia kuongeza fursa za elimu kwa vijana wa Kitanzania na kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu nchini.

Hafla hiyo ya Futari imejumuisha viongozi wa taasisi za umma na za binafsi ambazo zinashirikiana kwa karibu na HESLB katika utekelezaji wa majukumu yake ya utoaji na urejeshaji wa mikopo ya wanafunzi katika vyuo vya kati na taasisi za elimu ya juu nchini.

Published: March 14, 2026 at 9:06 PM