Watumishi wanawake wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) leo (Jumapili, Machi 08, 2026) wameungana na maelfu ya wanawake kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika Viwanja vya Barafu Mburahati, ambapo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo yaliyosheheni ujumbe wa haki, usawa na uwezeshaji wa wanawake.
Katika hotuba yake, Mhe. Chalamila amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki yanayowezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es salaam amesisitiza kuwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yana mchango mkubwa katika kujenga mshikamano, kuhamasisha usawa wa kijinsia na kuongeza fursa za uwezeshaji kwa wanawake katika nyanja mbalimbali.
“Maadhimisho haya yanatukumbusha kuwa wanawake ndio nguzo kubwa ya maendeleo na mambo mengi katika taifa letu. Tunapaswa kuyaona kama jukwaa la kuimarisha umoja, kujenga hamasa na kusukuma mbele agenda ya usawa wa kijinsia,” amesema, Mhe. Chalamila na kuwakumbusha wanawake kuwa wana wajibu mkubwa wa kujiimarisha kiuchumi kwa kufanya kazi kwa bidii na kutumia ipasavyo fursa zinazopatikana.
“Maadhimisho haya yatukumbushe kuwa wanawake tuna wajibu mkubwa sana wa kujiimarisha kiuchumi kwa kufanya kazi kwa juhudi. Kila mwanamke anapaswa kufanya mambo kulingana na uwezo na kipato chake, na si kuishi kwa kuiga maisha ya wengine,” amesisitiza Mhe. Chalamila.
Aidha, katika nasaha zake kwa jamii, amewataka wanaume na wanawake wanaopata mafanikio katika maisha yao kuhakikisha wanawakumbuka wazazi wao, hususan mama zao, kwa kuwasaidia na kuboresha maisha yao.
Kwa upande mwingine, Mkuu huyo wa Mkoa wa Dar es salaam amependekeza maboresho katika maadhimisho ya mwaka ujao kwa kufikiria kujumuisha kliniki maalum kwa ajili ya wanawake, itakayosaidia kutoa huduma mbalimbali za afya, ushauri na elimu kuhusu sharia na ustawi wa wanawake.
Awali, wakati wa utambulisho wa mgeni rasmi, Mhe. Albert Msando, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo alionesha furaha kwa Wilaya ya Ubungo kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo ya kimkoa.
“Tunajivunia kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya kwa Mkoa wa Dar es Salaam. Nawapongeza wanawake wote kwa mwonekano wao mzuri na ushiriki wao mkubwa katika tukio hili muhimu,” amesema Mhe. Msando.
Kwa upande wake, Suzane Kayange akisoma risala kwa niaba ya wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam, ameeleza changamoto zinazowakabili wanawake ikiwemo mzigo wa majukumu ya kifamilia na malezi, hali inayowazuia baadhi yao kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. Wanawake wa Dar es Salaam wameomba juhudi za pamoja kati ya serikali na jamii ili kuimarisha haki na usawa wa kijinsia.
Maadhimisho ya mwaka huu 2026 yamebeba kauli mbiu inayosisitiza haki, usawa na uwezeshaji wa wanawake na wasichana, ikikumbusha jamii kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila kuwapa wanawake nafasi sawa katika elimu, uchumi, uongozi na maamuzi ya kijamii.
Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 08 kila mwaka, imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuadhimisha mafanikio ya wanawake, kutathmini changamoto zilizopo na kuhamasisha jamii kushirikiana kuhakikisha wanawake wanapata haki, heshima na fursa sawa katika kujenga taifa lenye ustawi na maendeleo endelevu.