5
Mar 2026

Kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani 2026: HESLB Yagawa Taulo za Kike Temeke Sekondari

HESLB leo (Machi 05, 2026) imetembelea na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Temeke jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 08 Machi.

Akizungumza katika tukio hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Rasilimali Watu wa HESLB, Bi. Suzana Kiwelu amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuwapa moyo wanafunzi wa kike katika safari yao ya masomo pamoja na kuwapatia zawadi itakayowasaidia kusoma kwa furaha na kujiamini. Amesisitiza kuwa mabadiliko ya kibaiolojia wanayopitia wanafunzi wa kike ni ya kawaida na hayapaswi kuwa kikwazo katika kufikia ndoto zao za kielimu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Temeke, Bi. Ingia Mtenga ameishukuru HESLB kwa kuwakumbuka wanafunzi wa kike wa shule hiyo na kutoa zawadi hizo. Amesema taulo hizo zitakuwa chachu ya kuwahamasisha mabinti kusoma kwa bidii bila kukatishwa tamaa na changamoto zozote zinazoweza kuwazuia kuhudhuria masomo.

Sambamba na hilo, Mchumi kutoka HESLB, Bi. Neema Mkemwa amewahimiza wanafunzi kuelewa umuhimu wa usawa wa kijinsia na kuwahamasisha kuripoti katika dawati la jinsia iwapo watakutana na viashiria vya uvunjifu wa maadili shuleni au majumbani. Amesisitiza umuhimu wa kujenga jamii yenye upendo na heshima kati ya jinsia zote kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Naye Joyce James, mwanafunzi wa kidato cha tano katika shule hiyo, ameishukuru HESLB kwa kuwajali na kuahidi kuwa wanafunzi wataongeza juhudi katika masomo yao ili kuleta matokeo chanya.

Katika tukio hilo, jumla ya maboksi 105 ya taulo za kike yenye thamani ya shilingi milioni 6 yametolewa kwa wanafunzi wa kike wa Shule ya Sekondari Temeke, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya jinsia ya HESLB pamoja na kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Shule ya Sekondari Temeke ina jumla ya wanafunzi 3,054 kuanzia kidato cha I hadi cha VI ambapo wasichana ni 1,530 na wavulana ni 1,524. Shule hiyo inafundisha masomo katika michepuo ya Sayansi, Sanaa na Biashara.

Kwa mwaka 2026, wanafunzi 778 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza huku wanafunzi 632 wakiwa tayari wameripoti shuleni, kati ya idadi hiyo, wanafunzi 474 ni wa mchepuo wa Sayansi.

Published: March 5, 2026 at 11:19 AM