Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), CRDB Bank Foundation na kampuni ya Basil Link zimeingia makubaliano rasmi ya ushirikiano yatakayolenga kuwawezesha wanafunzi wa vyuo vikuu kupata ujuzi wa kidigitali, elimu ya ujasiriamali na elimu ya fedha. Makubaliano hayo yamefikiwa leo, Februari 18, 2026 katika hafla fupi ya uzinduzi wa programu hiyo iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es Salaam.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Afisa Mkuu wa Fedha wa CRDB, Bw. Frederick Nshekanabo, ambaye alieleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kujenga kizazi chenye maarifa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya dunia ya kidigitali. Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Nshekanabo amesema, “Tunataka kujenga uchumi wa kidigitali ambao ni kichocheo muhimu cha maendeleo kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050.”
Aidha, aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kutumia fursa hiyo kikamilifu, ikiwemo kupata kompyuta ili kurahisisha kujifunza vyuoni. Aliongeza kuwa kupitia programu hiyo, wanafunzi watanufaika na elimu ya kifedha, mafunzo ya ujasiriamali, ushauri elekezi pamoja na fursa za mikopo nafuu. Alieleza kuwa kupitia ushirikiano na Bodi ya Mikopo, wataweza kuwafikia kwa urahisi zaidi wanufaika wa mikopo waliopo vyuoni na kuwaandaa kupitia program hiyo kwa maisha baada ya kuhitimu elimu zao.
Bw. Nshekanabo amewakumbusha vijana kuwa kuhitimu chuo pekee bila kuwa na mawazo ya ubunifu yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali haitoshi. Ameongeza kuwa fursa zitakazotolewa kupitia programu hiyo zitasaidia wahitimu kurejesha mikopo ya elimu ya juu kwa wakati, na hivyo kuwezesha vijana wengine kunufaika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upangaji na Utoaji Mikopo wa HESLB, Dkt. Peter Mmari, amesema HESLB ipo tayari kushirikiana na taasisi binafsi katika kujenga uchumi wa kidigitali na kuwawezesha vijana wa vyuo vikuu. Alieleza kuwa Serikali imewekeza kwa vijana kupitia elimu ya kati na ya juu kwa zaidi ya miaka 20, ambapo hadi sasa takribani TZS 8.2 trilioni zimetolewa kwa wanafunzi zaidi ya 830,000 ili kuwawezesha kufikia ndoto zao.
Dkt. Mmari amesisitiza umuhimu wa mashirikiano na taasisi mbalimbali, zikiwemo za binafsi, kupitia mifumo ya kidigitali ili kuwafikia wanufaika wa mikopo walioajiriwa na taasisi hizo na kurahisisha ukusanyaji wa mikopo. Amebainisha kuwa kwa sasa takribani TZS 220 bilioni hukusanywa kwa mwaka kutoka kwa wanufaika wa mikopo na kwamba HESLB ipo tayari kushirikiana na CRDB Bank Foundation na Basil Link ili kuhakikisha vijana wanapata elimu ya fedha ili kutumia vizuri mikopo yao, kuwa wabunifu na kuweza kujiajiri na kuajiri wengine baada ya kuhitimu masomo yao. Hatua hiyo hatimaye itawawezesha wanufaika kurejesha mikopo yao kwa wakati ili kugharimia vijana wengine wanaojiunga na vyuo.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Basil Link, Dkt. Basil Emmanuel, ametoa wito kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kujitokeza kwa wingi kushiriki katika programu mbalimbali zitakazoratibiwa chini ya ushirikiano huo. Ameeleza kuwa timu yao itaanza kutembelea vyuo vikuu mbalimbali ili kutoa elimu na mafunzo kwa wanafunzi kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kushindana katika soko la ajira na kujiajiri katika mazingira ya uchumi wa kidigitali.
Utekelezaji madhubuti wa makubaliano haya kwa pande zote tatu unalenga kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na kupanua wigo wa fursa zinazowafikia kwa wakati na kwa ufanisi. Wanafunzi watanufaika na ujuzi utakaowawezesha kufikia malengo yao ya kitaaluma na kiuchumi, na hivyo kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa.