Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


12
December 2023

KAMATI BARAZA LA WAWAKILISHI YAFURAHISHWA USHIRIKIANO HESLB, ZHELB

Jumanne, Disemba 11, 2023

Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imefanya ziara ya mafunzo katika ofisi ndogo za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jijini Dar es salaam na kupongeza ushirikiano wa kikazi kati ya HESLB na Bodi ya Mikopo ya Elimu Zanzibar (ZHELB).

Katika ziara hiyo, wajumbe wa Kamati wakiongozwa na Mwenyekiti Mhe. Sabiha Filfil Thani, walipokea taarifa ya utendaji iliyowasilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru ambaye aliwaeleza wajumbe kuwa mwezi Aprili, 2021 HESLB na ZHELB zilisaini Hati ya Makubaliano ili kuimarisha ushirikiano katika kubadilishana taarifa, uzoefu na ujuzi kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi wa taasisi hizo mbili.

“Kwenye Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB tuna wajumbe wawili kutoka Zanzibar walioteuliwa kwa mujibu wa sheria, lakini pia mwaka 2021 tulisaini ‘MoU’ na tunafanya kazi kwa karibu sana ili kuongeza tija na ufanisi kwa taasisi zote mbili … mwanafunzi hawezi kupata mkopo kutoka Bodi zote mbili,” amesema Badru.

Akiongea katika majumuisho, Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. Thani, alipongeza ushirikiano uliopo kati ya HESLB na ZHELB na kuongeza kuwa Kamati imefurahishwa na taarifa ya utendaji ambayo imewaongezea wajumbe uelewa wa masuala mengi kuhusu utoaji na urejeshaji mikopo na ruzuku.

“Tunashukuru sana kwa wasilisho la kina, limetuelimisha sana hususani kwa namna mnavyojitahidi kuongeza ufanisi kwa kutumia teknolojia … na katika mashirikiano yenu na ZHELB, tunawapongeza wote, HESLB na ZHELB endeleeni kushirikiana zaidi,’ amesema Mhe. Thani.

Kwa upande wake, mjumbe wa Kamati na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulgulam Hussein amesema, ni lengo la Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuona ZHELB na HESLB zinashirikiana kwa karibu ili huduma zinazotolewa na taasisi hizo ziwafikie watanzania wengi zaidi.