Higher Education Students' Loans Board

  • Dar es Salaam, Tanzania. P.O.Box 76068

  • General call +255 22 286 4643

  • Monday - Friday8:00am - 5:00pm

News & Events


26
June 2025

HESLB NA MUM WAZUNGUMZA

Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa alilotoa kwenye maadhimisho ya miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM) kuhusiano na kutoa elimu kuhusu utoaji wa mikopo, Jumatano Juni 25, 2025, ujumbe kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ulioongozwa na Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo, Bw. George Mziray ulikutana na kuzungumza na menejimenti ya MUM kuhusu namna bora ya kuhudumia wanafunzi, kuboresha mawasiliano na ushirikiano katika kazi.

Kikao hicho kilichoongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma (DVC - Academic) Prof. Hamza Mustafa Njozi, kilijadili kwa kina kuhusu changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wanafunzi wenye mahitaji maalum na kushauriana namna bora ya kuwasilisha changamoto hizo ili zipatiwe ufumbuzi mapema.

Naye Dkt. Hassan Mohammed Issa ambaye ni “Dean of Students” na mnufaika wa mkopo toka HESLB, alikuwa mjumbe kwenye kikao hicho ambapo ameishukuru serikali kupitia HESLB kwa kumuwezesha kusoma elimu ya juu na kuiomba HESLB kuendelea kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum na wale wanaotoka kwenye kaya masikini kupata kiwango kikubwa cha mkopo hasa kwenye upande wa ada.

Bw. Mziray alitoa ufafanuzi zaidi kuhusu vipaumbele vinavyotolewa na serikali katika utoaji mikopo hasa kwa waombaji wenye mahitaji maalum na kusisitiza kuendelea kushirikiana na vyuo katika kuwahudumia kwa karibu wanafunzi wenye mahitaji maalum.

HESLB na MUM zilikubaliana kuendelea kushirikiana, kufanya kazi kwa ukaribu katika kutatua changamoto za wanafunzi, pamoja na kuboresha mawasiliano ili kuongeza ufanisi katika utoaji na urejeshwaji wa mikopo.