Higher Education Students' Loans Board
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inapenda kuwafahamisha waombaji mkopo wa elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2023/2024 kuwa ‘Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Mwaka wa Masomo 2023/2024’ wenye maelezo ya kina ya vigezo na utaratibu wa maombi utapatikana katika www.heslb.go.tz kuanzia wiki ya kwanza ya mwezi Julai, 2023.
Taarifa hii inalenga kutoa ufafanuzi kwa wanafunzi waliofanya mitihani ya Taifa ya kidato cha sita mwezi Mei, 2023 ambao wamekua wakituma barua pepe na kufika katika ofisi zetu kupata ufafanuzi.
Aidha, kwa sasa, waombaji mikopo watarajiwa wanashauriwa kujiandaa kwa kuhakikisha yafuatayo:
i. Kuwa na akaunti ya benki yenye jina sawa na kwenye cheti chake cha kidato cha nne;
ii. Kuwa na namba ya simu iliyosajiliwa kwa jina lake ambayo ataitumia akiwa chuoni;
iii. Kuhakiki cheti chake cha kuzaliwa kwa kufuata maelekezo ya RITA (Tanzania Bara) au ZCSRA (Zanzibar);
iv. Kuandaa nakala ya kitambulisho cha mdhamini wake; kinaweza kuwa kimoja kati ya NIDA, Kadi ya Mpiga Kura, Leseni ya Udereva, Pasi ya Kusafiria, au Kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi;
v. Kuandaa picha ndogo za rangi (pass-port size) za mwombaji mkopo na mdhamini wake; na
vi. Kuandaa namba ya NIDA. Kama mwombaji hana kwa sasa, haitamzuia kufanya maombi ya mkopo.
Aidha, tunapenda kuwafahamisha waombaji mkopo watarajiwa kuwa watakuwa na muda wa kutosha wa siku 90 wa kuomba mkopo. Hivyo, kwa sasa wanashauriwa kuandaa nyaraka muhimu ili kurahisisha uombaji mkopo mara dirisha litakapofunguliwa mwezi Julai, 2023.
Imetolewa na:
Mkurugenzi Mtendaji,
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB),
Juni 2, 2023