2
Sep 2026

Dkt. Kiwia Aishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB Inayomaliza Muda Wake

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia, ametoa shukrani za dhati kwa Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB inayomaliza muda wake, akieleza kuwa ushirikiano mzuri na uongozi wa Bodi hiyo umeiwezesha HESLB kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yake ya kimkakati katika kipindi cha miaka mitatu (2023-2026).

Dkt. Kiwia ametoa shukrani hizo wakati wa hafla fupi iliyoambatana na vikao maalum kati ya Menejimenti ya HESLB na Bodi ya Wakurugenzi vilivyofanyika tarehe 01 na 02 Septemba, 2026 katika Hoteli ya Malaika jijini Mwanza.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kiwia amesema Bodi hiyo imekuwa ya kipekee kutokana na ushirikiano wake wa karibu na Menejimenti, jambo lililowezesha HESLB kutekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuongeza ufanisi ikiwemo utoaji wa mikopo na kuhakikisha wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji wanapata fursa ya kupata elimu ya juu.

“Kwa niaba ya Menejimenti na watumishi wote wa HESLB, ninawashukuru kwa dhati Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kwa ushirikiano wenu wa karibu, ushauri na uongozi mlioutoa katika kipindi chote cha uongozi wenu. Bodi hii imekuwa ya kipekee na imeiwezesha HESLB kutekeleza mikakati muhimu ya kuongeza idadi ya wanafunzi wanaonufaika na mikopo, huku tukijenga msingi wa kuwa na mfuko endelevu wa mikopo,” amesema Dkt. Kiwia.

Ameongeza kuwa, mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wa Bodi hiyo yenye wajumbe 9 wanaowakilisha maeneo ya sheria, fedha, elimu ya juu na elimu ya kati, ni matokeo ya ushirikiano, uongozi thabiti na maamuzi ya kimkakati yaliyolenga kuimarisha huduma zinazotolewa na HESLB kwa wanafunzi na wadau wake.

Dkt. Kiwia amewashukuru Wajumbe wa Bodi hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Hamisi Dihenga kwa kujitolea kwao, weledi na usimamizi madhubuti, akisema Menejimenti inathamini mchango wa kila mmoja katika kuhakikisha HESLB inatimiza dhamana yake ya kuwezesha wanafunzi wa Kitanzania kupata elimu ya juu kupitia mikopo na ruzuku.

Vikao maalum vya Menejimenti ya HESLB na Bodi ya Wakurugenzi vilivyofanyika tarehe 01 na 02 Septemba, 2026, vilitoa fursa kwa pande hizo kutathmini utekelezaji wa majukumu na mikakati mbalimbali ya HESLB, pamoja na kuhitimisha kipindi cha uongozi wa Bodi inayomaliza muda wake.

Hafla hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya kushukuru, kutambua, kuthamini na kuaga kwa heshima Bodi ya Wakurugenzi inayomaliza muda wake, huku Menejimenti ya HESLB ikieleza utayari wa kuendeleza misingi mizuri ya utendaji na mikakati iliyowekwa kwa manufaa ya wanafunzi na ustawi wa HESLB.

Published: September 2, 2026 at 5:42 PM