31
Aug 2026

KAMATI ZA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR ZAJIFUNZA UZOEFU HESLB

Wajumbe wa Kamati za Ustawi wa Jamii na Kamati ya Usimamizi wa Fedha (PSC) za Baraza la Wawakilishi Zanzibar, leo Agosti 31, 2026 wamefanya ziara katika ofisi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kujifunza na kupata uzoefu wa utekelezaji wa majukumu katika eneo hilo la Sekta ya elimu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii, Mhe. Hussein Ibrahim Makungu, amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza namna HESLB inavyosimamia fedha za elimu, matumizi ya teknolojia na mfumo wa urejeshaji wa Mikopo pia ameipongeza HESLB kwa kazi nzuri inayoifanya. 

Katika ziara hiyo, wajumbe hao wamepata fursa ya kufahamu namna HESLB inavyosimamia utoaji wa mikopo na ufadhili wa wanafunzi, urejeshaji wa mikopo na matumizi ya mifumo ya kidigitali katika kuboresha huduma.

Awali, akitoa wasilisho kuhusu muundo na utekelezaji wa majukumu ya HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Dkt. Bill Kiwia, amesema HESLB ilianzishwa mwaka 2004 kwa Sheria na inatekeleza majukumu makuu mawili ambayo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye uhitaji pamoja na kukusanya fedha kutoka kwa wanufaika ambao madeni yao yameiva.

Dkt. Kiwia amesema kwa mwaka wa masomo 2026/2027, serikali imetenga TZS 1.07 trilioni kwa ajili ya mikopo na ufadhili, unaolenga kuwanufaisha wanafunzi 292,463, wakiwemo wanafunzi wapya na wanaoendelea na masomo.

Wengine waliondamana na Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati hizo mbili za Baraza la Wawakilishi Zanzibar ni pamoja na viongozi wa taasisi na maafisa wa Wizara ya Elimu ya Muungano (WyEST) na Wizara ya Elimu Zanzibar (WEMA) wakiongozwa na Naibu Waziri wa WEMA, Mhe. Khadija Salum Ali ambaye amesema ziara hiyo imekuwa ya manufaa makubwa.

“Waheshimiwa Wenyeviti na Wawakilishi, nadhani mmeona faida ya ziara hii … tulivyokuja sivyo tutakavyoondoka”, amesema Mhe. Khadija.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za kujifunza na kubadilishana uzoefu katika usimamizi wa sekta ya elimu, ambapo Wajumbe wameeleza kuwa maarifa waliyoyapata HESLB yatakuwa sehemu ya uzoefu watakaotumia katika kuimarisha usimamizi wa elimu na rasilimali zake Zanzibar.

Published: August 31, 2026 at 5:25 PM