28
Aug 2026

BoT NA HESLB WAZINDUA MWONGOZO WA UFADHILI WA KUMBUKUMBU YA NYERERE

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mhe. Emmanuel Tutuba kwa kushirikiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Dkt. Bill Kiwia wamezindua Mwongozo wa Ufadhili wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, unaolenga kuwawezesha wanafunzi mahiri wa Kitanzania kupata shahada ya uzamili katika fani muhimu za maendeleo ya Taifa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika leo (Agosti 28, 2026) jijini Dar es Salaam, Gavana wa BoT, amesema mpango huo unalenga wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika Shahada ya Kwanza na Shahada ya Uzamili, hususan katika fani za Hisabati na Sayansi.

Amesema katika mwaka wa masomo 2025/2026, BoT ilitoa ufadhili kwa wanafunzi 100, huku kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ikitarajiwa kutoa ufadhili kwa wanafunzi 10, wakiwemo watatu wa Shahada ya Uzamili na saba wa Shahada ya awali.

Gavana Tutuba amesema BoT itaendelea kutunisha mfuko huo kwa lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi watakaonufaika na ufadhili huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwekeza katika elimu na rasilimali watu nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, amesema kukabidhiwa kwa jukumu la kutangaza na kupokea maombi ya ufadhili huo ni ishara ya imani ambayo BoT imejenga kwa taasisi hiyo kutokana na uwezo wake wa kusimamia ufadhili wa wanafunzi kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji.

Dkt. Kiwia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa fursa za elimu, akisema HESLB imeendelea kuwekeza katika mifumo ya kidijitali inayomwezesha mwanafunzi kuomba ufadhili kwa muda mfupi na kwa urahisi zaidi.

Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, wanafunzi watakaochaguliwa watapatiwa ufadhili wa asilimia 100, unaogharimia gharama za moja kwa moja za masomo pamoja na mahitaji ya mwanafunzi kwa kuzingatia muundo wa gharama wa taasisi husika.

Ameeleza kuwa maombi ya ufadhili huo yatafanyika kupitia Mfumo wa Maombi ya Mikopo wa HESLB (OLAMS) kuanzia Septemba 5 hadi Oktoba 5, 2026.

Ufadhili huo ulianzishwa na BoT mwaka 2009 kwa lengo la kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kuendeleza dhamira yake ya kutumia elimu kama nyenzo muhimu ya kujenga rasilimali watu na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Mpango huo pia unaendelea kuakisi umuhimu wa kuwekeza katika vijana wenye uwezo wa kitaaluma katika fani zinazohitajika kwa maendeleo ya Tanzania, huku ushirikiano kati ya BoT na HESLB ukiwa na lengo la kuhakikisha fursa hizo zinawafikia wanafunzi wanaostahili kwa njia ya uwazi, ufanisi na inayotumia teknolojia.

Published: August 28, 2026 at 1:52 PM