20
Aug 2026

KM - WIZARA YA ELIMU AIPONGEZA HESLB KWA ELIMU NA MAKUSANYO YA MIKOPO ILIYOIVA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, leo (Alhamisi, Agosti 20, 2026) ametembelea banda la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yanayoendelea katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Tanga.

Akiwa katika banda hilo, Prof. Nombo ameipongeza HESLB kwa juhudi inazozifanya katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna sahihi ya kuomba mikopo ya elimu ya juu, pamoja na kuelimisha wanufaika kuhusu umuhimu wa kurejesha kwa wakati mikopo iliyoiva.

Aidha, Prof. Nombo ameipongeza HESLB kwa mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa marejesho ya mikopo, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha Mfuko wa Mikopo unaendelea kuwa endelevu na kuwafikia wanafunzi wengi zaidi wenye uhitaji.

“Hongereni sana kwa makusanyo makubwa katika mikopo iliyoiva. Kwa kweli mnastahili pongezi kubwa sana,” amesema Prof. Nombo.

Prof. Nombo pia amesisitiza umuhimu wa HESLB kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia maonesho na majukwaa mbalimbali ili kuongeza uelewa kuhusu fursa za mikopo, taratibu za maombi na wajibu wa wanufaika kurejesha mikopo yao kwa wakati.

Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 yalianza Agosti 15, 2026 na yanatarajiwa kuhitimishwa Agosti 24, 2026, yakilenga taasisi na wadau wa elimu kuonesha huduma, ujuzi na ubunifu ili kutangaza fursa zinazopatikana katika sekta ya elimu.

Published: August 20, 2026 at 6:59 PM