18
Aug 2026

Prof. Mkenda Afungua Rasmi Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Jijini Tanga

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda leo (Agosti 18, 2026) amefungua rasmi Maonesho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, Jijini Tanga.

Mhe. Prof. Mkenda amemwakilisha Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ambapo pia viongozi mbalimbali wamehudhuria hafla hiyo ya ufunguzi akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian ambaye amewakaribisha wageni kutembelea vivutio mbalimbali vilivyomo mkoani humo ukiutaja Tanga kuwa ni ‘lango la biashara la nchi za Afrika Mashariki na SADC’.

Maonesho hayo yanayolenga kuhamasisha na kuonesha mchango wa elimu, ujuzi na ubunifu katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa, yalianza Agosti 15, 2026 na yanatarajiwa kufikia tamati Agosti 24, 2026, yakiwa na kauli mbiu isemayo: “Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inashiriki kwa kutoa elimu na uelewa kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu huduma inazotoa, hususan namna sahihi ya kuomba mikopo ya elimu ya juu pamoja na urejeshaji wa mikopo iliyoiva.

Ushiriki wa HESLB unalenga kuwafikia wanafunzi, wazazi, walezi na wananchi kwa ujumla ili kuwapatia taarifa sahihi kuhusu fursa za mikopo ya elimu ya juu, taratibu za maombi pamoja na wajibu wa wanufaika katika kurejesha mikopo yao kwa wakati.

Aidha, maonesho hayo yanatoa fursa kwa taasisi mbalimbali za elimu, wadau wa sekta ya elimu, wanafunzi na wananchi kukutana, kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo ya elimu, ujuzi na ubunifu nchini.

HESLB inaendelea kuwakaribisha wananchi na wadau mbalimbali kutembelea banda lake katika maonesho hayo ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, ili kupata elimu na ufafanuzi kuhusu uombaji wa mikopo ya elimu ya juu na urejeshaji wa mikopo iliyoiva.

Published: August 18, 2026 at 9:00 PM