8
Aug 2026

MAMA SAMIA AFUNGA RASMI MAONESHO YA NANENANE DODOMA

Maonesho ya 33 ya Nanenane yamefungwa rasmi leo jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku yakihitimisha wiki ya maonesho yaliyokutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na maendeleo.

Akifunga maonesho hayo, Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha sekta ya kilimo na kuhakikisha Watanzania wanatumia kikamilifu fursa zilizopo ili kuongeza tija na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Katika maonesho hayo, HESLB ilishiriki kikamilifu, ikitumia jukwaa hilo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma hususan fursa za mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2026/2027.

Ushiriki wa HESLB umewapa wananchi fursa ya kupata ufafanuzi wa moja kwa moja kuhusu taratibu za maombi ya mikopo, vigezo vinavyotumika pamoja na elimu ya Urejeshaji mikopo chechefu.

Mbali na ushiriki katika maonesho ya kitaifa yaliyofanyika Dodoma, HESLB pia imeendelea kushiriki katika maonesho ya Nanenane katika kanda mbalimbali nchini, hatua iliyolenga kusogeza huduma na elimu kuhusu mikopo ya elimu ya juu karibu zaidi na wananchi.

Kupitia ushiriki huo, wananchi katika maeneo mbalimbali wamepata fursa ya kukutana na wataalamu wa HESLB, kuuliza maswali na kupata elimu kuhusu masuala yanayohusu mikopo na huduma zitolewazo na Bodi.

Aidha maonesho ya Nanenane yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kukutanisha Serikali, taasisi mbalimbali, sekta binafsi, wakulima, wafugaji, wajasiriamali na wananchi kwa ujumla, yakitoa nafasi ya kuelimishana, kuonesha bidhaa na huduma pamoja na kujenga mahusiano ya kibiashara na kijamii.

Mama Samia amefunga rasmi maonesho hayo akiacha ujumbe wa kuwa wazalendo katika kazi na kufanya bidii zaidi ili kuleta Tija na kutekeleza Dira ya 2050.

Published: August 8, 2026 at 7:05 PM