6
Aug 2026

Ulega: Bajeti ya Trilioni 1.07 ya Mikopo ya Elimu ya Juu ni Fursa kubwa kwa Vijana

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah H. Ulega (Mb), ameipongeza HESLB kwa kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea mkoani Morogoro.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la HESLB, Mhe. Ulega amesema ushiriki wa HESLB katika maonesho unatoa fursa muhimu kwa wananchi kupata elimu kuhusu huduma za mikopo ya elimu ya juu, vigezo vya ufadhili pamoja na taratibu za uombaji wa mikopo.

Mhe. Ulega amepongeza juhudi za Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kuwekeza katika elimu kupitia ongezeko kubwa la bajeti ya mikopo ya elimu ya juu.

Amesema ongezeko la bajeti ya mikopo kutoka Shilingi bilioni 570 mwaka wa fedha 2021/2022 hadi Shilingi trilioni 1.07 mwaka wa fedha 2026/2027, ni hatua kubwa itakayowezesha vijana wengi zaidi wenye sifa na uhitaji kupata fursa ya kujiunga na elimu ya juu.

“Ongezeko hili la bajeti linaonesha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha hakuna kijana mwenye sifa anayekosa fursa ya elimu ya juu kutokana na changamoto za kifedha,” amesema Mhe. Ulega.

Aidha, amepongeza HESLB kwa kupanua wigo wa utoaji wa mikopo hadi ngazi ya Diploma, hatua aliyoeleza kuwa itaongeza upatikanaji wa elimu ya ufundi na ujuzi kwa Watanzania, sambamba na kuendelea kutekeleza Mpango wa Ufadhili wa Samia unaolenga kuibua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi wenye ufaulu wa juu zaidi.

Katika hatua nyingine, ameishauri HESLB kuendelea kutumia mifumo ya kidijitali na teknolojia za kisasa ili kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi na kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.

“Matumizi ya teknolojia ni njia muhimu ya kuboresha huduma, kuongeza uwazi na kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma kwa haraka na kwa urahisi,” amesisitiza.

HESLB inaendelea kushiriki katika Maonesho ya Nanenane kwa kutoa elimu kuhusu huduma zake mbalimbali, ikiwemo mikopo ya elimu ya juu, urejeshaji wa mikopo, Mpango wa Ufadhili wa Samia na huduma nyingine zinazolenga kuwawezesha Watanzania kupata elimu na kukuza rasilimali watu.

Published: August 6, 2026 at 4:13 PM