4
Aug 2026

HESLB NA NCAA WAZINDUA MWONGOZO WA NGORONGORO SCHOLARSHIP

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) leo Agosti 04, 2026 imezindua rasmi Mwongozo wa Utoaji wa Ngorongoro Scholarship, hatua inayoweka msingi wa kuanza kwa utoaji wa ufadhili maalum wa elimu ya juu kwa wanafunzi wanaotoka katika jamii zinazoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro kuanzia mwaka wa masomo 2026/2027.

Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari katika Ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema uzinduzi huo ni utekelezaji wa Makubaliano ya Ushirikiano (MoU) yaliyosainiwa kati ya HESLB na NCAA tarehe 24 Oktoba, 2025, yenye lengo la kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wa Ngorongoro.

"Kuanzia mwaka wa masomo 2026/2027, HESLB kwa kushirikiana na NCAA itaanza kutoa ufadhili maalum wa elimu ya juu kwa wanafunzi wanaotoka katika jamii zinazoishi ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro. Hatua hii ni uwekezaji muhimu katika rasilimali watu na maendeleo endelevu ya Taifa kupitia elimu," amesema Dkt. Kiwia.

Alieleza kuwa, katika awamu ya kwanza, wanafunzi 15 watanufaika na ufadhili huo huku NCAA ikitenga TZS milioni 99 kugharamia masomo yao. Aliongeza kuwa mwongozo huo umeweka vigezo na taratibu za utoaji wa ufadhili, huku dirisha la maombi likitarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 15 Agosti, 2026 kupitia mfumo wa kidijitali ulioboreshwa na HESLB.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa NCAA, Bi. Gloria Bideberi, amesema mpango huo unaonesha dhamira ya NCAA ya kuwekeza katika maendeleo ya jamii kupitia elimu sambamba na kuimarisha juhudi za uhifadhi.

"Ngorongoro Scholarship inaashiria dhamira ya NCAA ya kuwekeza katika rasilimali watu kupitia elimu. Tunaamini maendeleo ya uhifadhi hayawezi kutenganishwa na maendeleo ya watu, ndiyo maana tumeamua kushirikiana na HESLB kuhakikisha kila mwanafunzi anayekidhi vigezo anapata fursa ya kufadhiliwa," amesema Bi. Bideberi.

Alibainisha kuwa NCAA imekuwa ikiwezesha elimu kwa watoto wa jamii za Ngorongoro kwa zaidi ya miongo mitatu, ambapo hadi mwaka wa fedha 2025/2026 zaidi ya wananchi 15,000 walikuwa wamepatiwa ufadhili katika taaluma mbalimbali. Aidha, alisema kupitia Ngorongoro Fund yenye kaulimbiu "Elimu Endelevu kwa Maendeleo ya Jamii na Uhifadhi," ufadhili utaanza kwa wanafunzi wa fani zinazohusiana na uhifadhi wa wanyamapori, misitu, malikale na utalii, huku wigo ukitarajiwa kupanuliwa kadri mfuko utakavyoendelea kukua.

HESLB na NCAA zimetoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa jamii na vijana kutumia fursa hiyo kwa kuwasilisha maombi mara tu dirisha litakapofunguliwa, huku pia zikizihamasisha taasisi mbalimbali na wadau wa maendeleo kuunga mkono mfuko huo ili kuongeza idadi ya wanufaika katika miaka ijayo.

Published: August 4, 2026 at 1:12 PM