Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo Julai 3, 2026, amepita na kusalimia watumishi wa Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wanaotoa huduma kwa wananchi katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF).
Leo ilikuwa ni siku ya ufunguzi rasmi wa maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, maarufu Sabasaba, jijini Dar es salaam, ambapo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa ameongozana na Rais wa Msumbiji Mhe. Daniel Francisco Chapo aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa maonesho hayo ambayo pia yanatumika kuadhimisha miaka 50 ya DITF.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Zanzibar (ZHESLB), Bi. Umrat Mohammed, ametembelea Banda la HESLB na kupokea maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa kidijitali na HESLB. Wataalamu wa HESLB walimueleza namna mifumo ya kidijitali inavyorahisisha utoaji wa huduma kwa waombaji wa mikopo, wanufaika, wadaiwa na wadau wengine, hatua inayochangia kuongeza ufanisi, uwazi na upatikanaji wa huduma kwa wakati.
Watumishi wa HESLB waliopo kwenye maonesho hayo, wanaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi kwa kutumia mifumo ya kidijitali, ikiwemo kutoa elimu kuhusu mikopo ya elimu ya juu, taratibu za maombi ya mikopo, urejeshaji wa mikopo, pamoja na kujibu maswali mbalimbali yanayohusu huduma zinazotolewa na bodi hiyo.
HESLB inaendelea kuwakaribisha wananchi kutembelea banda lake ili kupata huduma na elimu kuhusu shughuli zake hadi Julai 13, 2026 siku ambayo Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam yatahitimishwa.