2
Jul 2026

HESLB, CAMFED Zasaini Makubaliano Kupanua Fursa Elimu ya Juu

HESLB na Shirika la Campaign for Female Education Tanzania (CAMFED), leo Alhamisi Julai 2, 2026, zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha ushirikiano katika kuongeza upatikanaji wa rasilimali za kugharamia elimu ya juu kwa wanafunzi wenye uhitaji, hususan wasichana wanaotoka katika mazingira yenye changamoto za kiuchumi na kijamii.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika katika ofisi za CAMFED zilizopo Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema makubaliano hayo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutafuta mbinu bunifu za kuongeza vyanzo vya fedha vitakavyowezesha wanafunzi wengi zaidi kupata fursa ya elimu ya juu.

“Serikali kupitia HESLB imeendelea kutafuta mbinu bunifu za kuongeza vyanzo vya fedha vitakavyosaidia wanafunzi wengi zaidi wenye sifa na uhitaji kupata fursa ya kuendelea na elimu ya juu. Makubaliano tunayoyasaini leo ni sehemu ya jitihada hizo,” amesema Dkt. Kiwia.

Kwa mujibu wa Dkt. Kiwia, ushirikiano huo unalenga kuongeza upatikanaji wa fedha za kugharimia elimu ya juu, kupanua fursa kwa makundi yenye uhitaji mkubwa, kuongeza uelewa kuhusu huduma za HESLB, kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali, kubadilishana uzoefu wa kitaasisi na kujenga msingi wa ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

“Ushirikiano huu unaendana kikamilifu na dira yetu ya kuhakikisha hakuna mwanafunzi mwenye sifa anayekosa fursa ya elimu ya juu kwa sababu ya changamoto za kifedha,” amesisitiza Dkt. Kiwia na kuongeza kuwa, “Tunatarajia ushirikiano huu utafungua ukurasa mpya wa uwezeshaji wa elimu ya juu nchini. Kwa pamoja tunaweza kupanua fursa za elimu, kuwawezesha vijana wengi zaidi na kuchangia maendeleo endelevu ya Taifa letu,” amesema Dkt. Kiwia.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa CAMFED Tanzania, Bi. Anna Sawaki, amesema makubaliano hayo yanalenga kuwafikia watoto wengi zaidi wenye uhitaji wanaotoka katika mazingira magumu ili waweze kupata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu.

“Tumekuwa tukifanya kazi na Bodi ya Mikopo kwa miaka mingi, na hivyo huu ni mwendelezo wa kazi ambayo tayari tulishaanza kwa miaka kadhaa … tunaahidi kuwa watekelezaji wazuri wa makubaliano haya na kutafuta vyanzo vingine vya kuongeza ufadhili kwa wanafunzi wahitaji kadri hali itakavyoruhusu” amesema Sawaki.

Makubaliano kati ya HESLB na CAMFED yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili katika kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali za ziada, kuboresha uratibu wa programu za uwezeshaji wa wanafunzi na kuongeza fursa za elimu ya juu kwa vijana wengi zaidi nchini, hususan wanaotoka katika mazingira yenye changamoto za kiuchumi na kijamii.

Published: July 2, 2026 at 1:02 PM