Mkuu wa Mashirikiano na Wadau wa Kampuni ya VISA Kanda ya Kati na Mashariki mwa Ulaya, Mashariki ya Kati na Afrika (CEMEA), Bw. Athman Ali, leo Julai 1, 2026, ametembelea Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) zilizopo jijini Dar es Salaam, ambapo amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia.
Ujio wa kiongozi huyo wa VISA ulilenga kujadili fursa za ushirikiano kati ya HESLB na VISA katika kuboresha mifumo ya utoaji na usimamizi wa fedha za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kutumia teknolojia za kisasa za huduma za kifedha.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilijadili namna ya kutatua changamoto zinazohusiana na matumizi ya fedha za mikopo, hususan kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa wanufaika zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, ikiwa ni pamoja na kugharimia mahitaji muhimu ya masomo na ustawi wa mwanafunzi akiwa chuoni.
Aidha, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kutumia suluhisho za kidijitali zitakazoongeza uwazi, usalama na ufanisi katika usimamizi wa fedha za mikopo, sambamba na kuwajengea wanafunzi utamaduni wa matumizi sahihi ya huduma za kifedha.
Ushirikiano kati ya HESLB na VISA unatarajiwa kuibua fursa mpya za kuboresha utoaji wa huduma kwa wanufaika wa mikopo, kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa tija na kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha upatikanaji wa elimu ya juu nchini.