Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anayesimamia Utafiti, Prof. Nelson Boniface, ametembelea banda la Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea jijini Dar es salaam, na kueleza kufurahishwa na huduma mbalimbali za kidigitali zinazotolewa kwa wananchi.
Baada ya kupata maelezo kuhusu mifumo ya kidigitali inavyorahisisha utoaji wa huduma, Prof. Boniface ameipongeza HESLB kwa juhudi zake za kuendelea kuboresha na kutumia teknolojia, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanafunzi na wadau wengine.
Amesema juhudi hizo zina mchango mkubwa katika kuwawezesha vijana wa Kitanzania kutimiza ndoto zao za kupata elimu ya juu kwa kuwaondolea changamoto za upatikanaji wa huduma za mikopo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Timu ya HESLB iliyopo kwenye Banda la Karume, inaendelea kutoa elimu na huduma mbalimbali zinazohusiana na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika, huku wananchi wakihimizwa kutembelea banda hilo ili kupata taarifa na huduma kwa karibu.
Maonesho ya Biashara ya Kimataifa kwa mwaka 2026, yanayotimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, yalianza Juni 28, 2026 na yanatarajiwa kufungwa Julai 13, 2026 katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es salaam.
Wananchi wanakaribishwa kutembelea Banda la HESLB kupata huduma na elimu kuhusu masuala ya mikopo ya elimu ya juu kwa kipindi chote cha maonesho.