23
Jun 2026

Maonesho ya Utumishi wa Umma 2026 Yahitimishwa

  • Prof. Nombo Asisitiza Huduma kwa Waombaji Mikopo 2026/2027

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, leo Juni 23, 2026, amefunga rasmi Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma huku akisisitiza umuhimu wa uwajibikaji, uadilifu na utoaji wa huduma bora kwa wananchi ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi za umma.

Katika hafla ya kufunga maonesho hayo, Prof. Shemdoe pia amezindua mifumo miwili muhimu ya Serikali ambayo ni Mfumo wa GSD (Government Services Directory) ambao ni Daftari la Huduma za Serikali. Mfumo huo unaainisha huduma zote zinazotolewa na Serikali na kuweka wazi gharama, muda na mahitaji ya kupata huduma husika. Aidha, Prof. Shemdoe amezindua Mfumo wa NGAO unaolenga kuimarisha usalama wa taarifa za mtumiaji wa mifumo ya TEHAMA katika taasisi za umma.

Imeelezwa kuwa mfumo wa NGAO ulianza kutumika mwaka 2025 kwenye barua pepe na Masijala (e-office) na mpaka sasa zaidi ya taasisi 700 zinautumia, kwenye GSD hadi sasa taasisi 554 zimeshaingizwa kwenye mfumo huo. HESLB inatumia mifumo yote mitatu kikamilifu.

Katika hatua nyingine, viongozi kadhaa kutoka sekta ya elimu, wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, wametembelea banda la HESLB kupata taarifa na kutoa pongezi kwa maboresho mbalimbali ya kiutendaji.

Akiwa bandani hapo, Prof. Nombo alitaka kufahamu utaratibu unaotumiwa na HESLB kuwahudumia waombaji watarajiwa wa mikopo, hususan katika kutangaza miongozo ya uombaji, kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha waombaji wanapata taarifa sahihi kuhusu vigezo na taratibu za kuomba mikopo kwa wakati.

Prof. Nombo amepata maelezo ya kina kuhusu maandalizi ya mchakato wa utoaji wa mikopo ya wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2026/2027, na jinsi HESLB ilivyojiandaa kutoa huduma bora kwa waombaji Mikopo watarajiwa.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, (OUT) Prof. Alex Makulilo, ametembelea banda la HESLB na kupongeza maboresho mbalimbali yaliyofanywa katika mifumo ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi. Ameeleza kuwa maboresho hayo yamechangia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiwakabili wanafunzi na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa huduma.

HESLB imeshiriki kikamilifu katika Maonesho Wiki ya Utumishi wa Umma kwa siku nane mfululizo kuanzia Juni 16 hadi 23, 2026, ikitoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali kuhusu utoaji na urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu. Kupitia ushiriki huo, HESLB imepata fursa ya kukutana na wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na kupokea maoni, ushauri na mapendekezo yatakayosaidia kuboresha zaidi huduma zake kwa manufaa ya watanzania.

Published: June 23, 2026 at 5:58 PM